Adul-Malik al-Houthi aliyasema hayo katika hotuba yake iliyopeperushwa kwa njia ya televisheni siku ya Alhamisi jioni wakati makumi ya maelfu ya watu wa Iran wakimiminika katika mkoa wa kusini mashariki wa Kerman kutoa heshima kwa kamanda huyo mashuhuri.
Amesema: "Marekani ilimlenga Hajj Qassem Soleimani kwani alikuwa kikwazo kikubwa kwa mafanikio ya njama zake nyingi."
Aidha amebaini kuwa: "Shahidi Haj Qassem Soleimani na mwanajihadi mwenzake wa Iraq, Abu Mahdi Al-Muhandis, walikuwa na majukumu tofauti na muhimu katika kukabiliana na njama za Israel na Marekani.".
Kiongozi huyo wa Yemen pia alizungumzia matukio ya hivi majuzi katika eneo la Asia Magharibi.
Alishutumu shambulio la adui Muisraeli katika Hospitali ya Kamal Adwan, kituo cha mwisho cha matibabu kilichosalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, kama kitendo cha kukosa aibu na uhalifu mkubwa.
Aliashiria masaibu ya wafungwa wa Kipalestina, akiwaelezea kuwa ni makubwa kutokana na mateso, kunyimwa matibabu, unyanyasaji, na aina zote za dhuluma katika magereza ya Israel.
Al Houthi pia alikosoa Mamlaka ya Palestina kuhusu kampeni yake inayoitwa eti ya usalama katika Ukingo wa Magharibi, na kusema kwamba hatua hizo zinakuja pamoja na hujuma za kijeshi za Israel zinazoendelea katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.
Amesema matumaini ya mamlaka hiyo ya kufikia amani na Israel kupitia ushirikiano na mazungumzo ni udanganyifu mkubwa kwani utawala huo unatamka waziwazi kupinga kuasisiwa taifa huru la Palestina.
Kiongozi wa Ansarallah amesisitiza kuwa Marekani inaendelea kuzuia azimio lolote la kutaka kusitishwa kwa mapigano na utoaji wa haraka wa huduma muhimu na misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza.
Mkuu wa Ansarullah pia amelaani mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Yemen, akisema lengo kuu la utawala huo ghasibu ni kuitenga Gaza huku operesheni za jeshi la Yemen zinazoiunga mkono Palestina zikiendelea kutoa pigo kubwa kwa utawala huo ghasibu.
Amesisitiza kuwa vitendo vya uchokozi vya jeshi la Israel havitazuia azma ya Yemen katika kuunga mkono Palestina.
4257776