IQNA

Raeisi aendelea kupongezwa na viongozi wa dunia baada ya ushindi katika uchaguzi wa rais Iran

18:11 - June 20, 2021
Habari ID: 3474024
TEHRAN (IQNA) - Viongozi mbali mbali duniani wanaendelea kumtumia salamu za pongezi Sayyid Ebrahim Raeisi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika Ijumaa.

Raeisi alipata karibu asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo  na anatazamiwa kuchukua nafasi ya Rais Hassan Rouhani ambaye anamaliza muhula wake wa pili baada ya kushikilia nafasi hiyo kwa muda wa miaka minane.

Ubalozi wa Palestina mjini Tehran umetangaza kuwa Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametuma ujumbe wa kumpongeza Raeisi kwa ushindi wake huku akisisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa kirafiki wa Iran na Palestina.

Naye Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani amemtakia Raeisi mafanikio na pia ameelezea matumaini yake kuwa uhusiano wa Iran na Qatar utazidi kuimarika. Kwa upande wake Sultan wa Oman Haitham bin Tariq Aal Said amemtumia salamu za kheri na fanaka rais mteule wa Iran na kuwatakia Wairani ustawi na ufanisi.

Halikadhalika Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki pia amempongeza Raiesi kwa ushindi wake na kuelezea matumaini yake kuwa uhusiano wa Ankara-Tehran utaboreka katika kipindi cha rais mpya wa Iran. Aidha amesema atakuwa na furaha kupata fursa ya kuitembelea Iran kwa ajili ya mkutano wa Baraza la Ngazi za Juu la Ushirikiano wa Iran na Uturuki punde baada ya janga la COVID-19 kumalizika. Pia Abdullah Abdullah, mwenyekiti wa Baraza Kuu la Maelewano Afghanistan naye pia amempongeza Raeisi kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Iran.

Rais wa Venezuela Nicholas Maduri halikadhalika naye ametuma ujumbe akimpongeza Raeisi kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais hapa nchini na ametoa wito wa kuboreshwa zaidi uhusiano kati ya nchi mbili.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi naye pia ametumia salamu za pongezi Raeisi kufuatia ushindi wake huku akisema atashirikiana naye kuboresha uhusiano mzuri ulioko baina ya Iran na India.

Rais Vladimir Putin wa Russia katika ujumbe wake wa pongezi kwa Raeisi amesema Iran na Russia zina uhusiano mzuri wa kirafiki na kijirani. Ameelezea matumaini yake kuwa katika kipindi cha urais wa Raeisi, kutashuhudiwa kuimarika uhusiano baina ya nchi mbili na pia katika uga wa kimataifa.

Viongozi wengine waliompongeza Rais mteule Raeisi ni pamoja na Rais Bashar al Assad wa Syria, Rais Barahm Salih wa Iraq, Waziri Mkuu Imran Khan wa Pakistan, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Khalifa bin Zayed Aal Nahyan, Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan Ilham Aliyev na Rais wa Armenia Armen Sargsyan.

3474989

Kishikizo: iran ، raeisi ، uchaguzi
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :