IQNA

Kwa mnasaba wa Maulidi
12:10 - October 19, 2021
News ID: 3474443
TEHRAN (IQNA)- Tuko katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama Maulidi.

Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu. Kwa hivyo wiki hii ni fursa munasibu ya kukutana na kuchunguza udharura wa daima wa kuwepo umoja wa Kiislamu hasa katika kipindi hiki cha fitina na ghasia. Waislamu wa madhehebu mbali mbali wanahitilafiana kuhusu baadhi ya masuala lakini wana nukta nyingi za pamoja kwani wote wana imani sawa kuhusu nukta za kimsingi kama vile Tauhidi au kuabudu Mungu Mmoja, Qur'ani Tukufu, Mtume na qibla.

Aidha wana mtazamo sawa kuhusu utekelezwaji wa ibada muhimu kama vile Sala, Saumu, Hija, Zaka n.k. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za pongezi, kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja ambayo inasadifiana na kuzaliwa Mtumu Mtukufu wa Uislamu. Tunawakaribisha kusikiliza makala hii fupi tuliyowaandalia kuhusu msingi wa umoja katika Qur'ani na Sira ya Mtume wa Uislamu SAW.

Qur’ani na umoja wa Kiislamu

 Tukiangazia Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume SAW, tutaona kuwa katika vyanzo hivyo viwili vyenye thamani kubwa zaidi katika Uislamu kumetiliwa mkazo mkubwa umoja wa Waislamu. Qur'ani Tukufu katika aya kadhaa imesisitiza kuhusu umoja na kuutaja kuwa ni neema kubwa. Katika Surat Al-I'mran aya ya 103, Allah SWT anasema: "Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka."

Katika aya hiyo Mwenyezi Mungu SWT anazungumzia kuhusu kushikamana na kamba yake. Katika tafsiri nyingi, misdaki ya wazi kabisa ya kamba hii imara imetajwa kuwa ni Qur'ani Tukufu. Allama Tabatabai kati ya mufasirina wakubwa wa Qur'ani ameandika hivi: "Habl (kamba) ya Mwenyezi Mungu ni Qur'ani iliyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu… Kushikamana hapa kusudio lake ni kushikamana na Aya za Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume wake, yaani kufungamana na Kitabu (Qu'rani) na Sunna ambapo kwa kufuata viwili hivyo, kunakuwepo dhamana na kuongoka."

Kushikamana Waislamu na Kitabu cha Allah SWT kwa kudumisha umoja baina yao kumefananishwa na mtu ambaye anapita katika njia hatari sana ambapo anakabiliwa na hatari ya kuanguka katika bonde lenye kina kirefu na hivyo daima anahofia kuanguka, lakini iwapo atashikilia kwa nguvu kamba zilizo katika pande mbili , ataweza kupita eneo hilo hatari na kufika alikokusudia. Ni kwa sababu hii ndio katika Qur'ani Tukufu mifarakano ikatajwa kama ukingoni mwa shimo la Moto. Katika aya tuliyoitaja hapo juu, Mwenyezi Mungu anawataka Waumini wakumbuke zama chungu za mifarakano na machafuko. Ukumbusho huo unatolewa ili Waislamu wapate hima ya kudumisha umoja.

Hii ni kwa sababu moja kati ya faida za umoja katika jamii ni kudumishwa amani, utulivu na usalama na kuwa mbali na vita na umwagaji wa damu. Kwa msingi kuwa kushukuru na kuilinda neema hii ya Mwenyezi Mungu ni moja kati ya majukumu muhimu ya Waislamu wote. Ni wazi kuwa kuibua fitina na mifarakano baina ya Waislamu ni jambo ambalo linaweza kutajwa kuwa sawa na kukufuru neema kubwa ya Mwenyezi Mungu.

Msifarakiane

Mwenyezi Mungu SWT katika Aya ya 105 ya Surat Al I'mran pia anatahadharisha Waislamu kwa kusema: Wala msiwe kama wale waliofarikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa." Qur'ani Tukufu pia inatoa wito kwa Waislamu wote watambuane kama ndugu. Katika aya ya 10 ya Surat Al H'ujuraat Mwenyezi Mungu SWT anasema: Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe." Ayah hii inawataka Waislamu waishi pamoja kama ndugu katika imani na wawe na mwenendo ambao utadumisha mfungamano na mshikamano wao ili kwa njia hiyo wawezu kuvutia rehema za Mwenyezi Mungu.

Kwa mtazamo jumla, Qu'rani Tukufu inataka kuwaleta pamoja wanaadamu wote duniani. Qur'ani inatoa wito wa umoja wa watu wote wa kitabu au Ahul Kitab na dini za mbinguni. Inawataka wawe chini ya kivuli cha kauli na itikadi moja na Waislamu na wawe na umoja. Katika Aya ya 60 ya Surat Al I'mran, Allah SWT anasema: Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.'

Ayah hii inataja Tauhidi kuwa chimbuko la mshikamano wa dini mbali mbali na inawataka wafuasi wa dini hizo kuja pamoja katika mhimili huo ili jamii iwe na utulivu. Hakuna shaka kuwa Waislamu ni chimbuko kuu la mshikamano huu na hivyo wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika hilo.

Kulinda nguzo za jamii ni kati ya taathira nzuri za umoja ulioashiria katika Qur'ani Tukufu. Wakati jamii inapojiepusha na mifarakano na kushikamana, basi hakutakuwa na pengo la adui kuingia na kuvuruga jamii kama hiyo. Tab'an umoja na mashikamano wa Waislamu utaweza kupatikana tu kwa kuwepo kiongozi mmoja wa Ummah. Katika sehemu ya Aya ya 46 ya Surat al-Anfaal tunasoma kuwa: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu.

Mhimili wa umoja

Mwenyezi Mungu SWT amemtaja Mtume wake kuwa ni mhimili wa umoja wa kivitendo baina ya Waislamu. Mhimili huu unajumuisha maneno na vitendo vyote vya Bwana Mtume SAW. Kwa hakika Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW alikuwa mlinganiji wa kwanza wa umoja wa Kiislamu na ili kufikia lengo hilo alistahamili masaibu na machungu mengi. Mara kwa mara alikuwa akionya kuhusu hatari zinazoukabili umma wa Kiislamu. Historia ya Uislamu inashuhudia namna Bwana Mtume SAW alivyojitahidi kuzuia mifarakano sambamba na kuimarisha safu za Waislamu. Alitumia faida za umoja kwa maslahi ya Uislamu na kuimarisha misingi ya kisiasa na kijamii katika umma wa Kiislamu.

Baada ya kuhamia Madina, Mtume Mtukufu wa Uislamu aliyaleta pamoja makundi mbali mbali kupitia utiwaji saini mikataba. Mikataba hii inaweza kutajwa kuwa moja kati ya njia za wazi kabisa za kuleta umoja katika jamii. Mkataba wa kwanza ulikuwa baina ya Mtume na makabila na kaumu zilizokuwepo Madina. Tadbiri na busara hii ilikuwa njia bora zaidi iliyokuwepo ya kuleta umoja wa kitaifa na mshikamano wa kidini. Kati ya ubunifu muhimu zaidi wa Mtume katika uga wa Umoja ni kuleta mshikamano wa kijamii baina ya Waislamu na kuwaunganisha kama ndugu. Mikataba hiyo ilijengeka katika kupinga ukabila na ukaumu na mkabala wake kuhimiza imani ya pamoja na mshikamano wa kijamii. Mtume SAW alileta muafaka na mkataba wa udugu baina ya Muhajirin au waliohajiri kutoka Makka na wenyeji wa Madina yaani Ansar.

Kwa kuwepo mshikamano huo wa kidugu baina ya Waislamu, Mtume wa Uislamu aliondoa uaadui uliokuwa umebaki miongoni mwa Waislamu tokea zama za Ujahili na kubadilisha hali hiyo kuwa ya kurehemeana na upendo. Mkataba wa udugu haukuja kwa dinari au thamani za kifedha bali mkataba huo ulikuwa umejawa na imani ya kimaanawi. Kama ambavyo Qur'ani Tukufu inavyosema katika Sura Anfal Aya ya 63: 'Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.'

Mtume SAW alisambaratisha mifarakano

Fikra asili ya Mtume SAW ilikuwa ni kuwauganisha Waislamu katika safu zao na kuondoa kila aina ya shubha ambayo ingeweza kuwasha moto wa chuki na uhasama uliokuwapo huko nyuma. Kwa msingi huo aliweza kuwaungaisha na kuleta mahaba miongoni mwa Waislamu kupitia muafaka wa udugu.

Mtume SAW alifanikiwa kusambaratisha vigezo vilivyokuwa vikileta mifarakano katika zama za ujahilia na mahala pake kuchukuliwa na mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Kwa msingi huu kupambana na taasubu na kupinga ubaguzi wa rangi na ukabila ni kati ya mbinu muafaka zilizotumiwa na Mtume SAW katika kuleta umoja wa Waislamu. Mtume SAW alipinga kujifaharisha kwa rangi ya ngozi na ukabila na alisema: "Iwapo katika moyo wa mtu kutakuwa na tone la kujifakharisha kikabila, Mwenyezi Mungu atamhuisha siku ya Kiyama akiwa na Waarabu wa zama za Jahiliya."

Kwa mtazamo wa Mtume SAW kukiuka mipaka na haki za watu wengine na kuvuruga utulivu ni moja ya sababu kuu ambazo hupelekea kuibuka mifarakano na utengano. Kwa msingi huo Bwana Mtume SAW aliwataka Waislamu kuhuisha moyo wa udugu na kupinga dhulma kwa kusema: "Mwislamu ni Ndugu ya Mwislamu. Hadhulumu, hamlaani wala kumtukana (Mwislamu mwenzake)."

Mtume Mtukufu wa Uislamu hata katika wasia wake, aliutahadharisha Umma wa Kiislamu kwa kusema: "Enyi watu, sikilizeni maneno yangu. Sijui, pengine sitawaona baada ya hapa. Enyi watu mumeharamishiwa kumwaga damu au kuchukua mali za wenzenu. Mfahamu kuwa kila Mwislamu ni ndugu ya Mwislamu mwingine na Waislamu ni ndugu baina yao."

Leo ambapo ni fakhari kwa Waislamu wote kufuata Qur'ani na kumfuata shakhsia mkuu wa Uislamu, Mtume Muhammad SAW, inastahiki kuona Waislamu wote wakiegemea katika nukta za kidini zinazowaleta pamoja ili kwa mara nyingine tushushudie ufanisi na mafanikio ya Waislamu kote duniani.

Chanzo: IRIB

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: