IQNA

Sura za Qur'an/13

Surat Ar-Ra’ad, kutukuzwa kwa Mwenyezi Mungu katika anga

13:54 - June 27, 2022
Habari ID: 3475432
TEHRAN (IQNA) – Mungurumo wa radi angani ni miongoni mwa alama za ukuu wa Mwenyezi Mungu na, kwa mujibu wa aya ya 13 ya Sura Ar-Ra’ad, inamtakasa na kumhimidi Mwenyezi Mungu.

Surah Ar-Ra’ad au ngurumo, ni sura ya 13 ya Qur'ani na sura ya 96 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW) na ina aya 43 na iko katika Juzuu ya 13 ya Kitabu kitukufu. Lengo la Sura ni kusisitiza nguvu ya ukweli na udhaifu wa uwongo. Kuna tofauti za maoni kuhusu kama ni Sura ya Makki au Madani (yaani iliteremshwa kwa Mtukufu Mtume huko Makka au Madina). Wengine wanasema ni Makki kwa sababu ya maudhui yake huku wengine wakisema kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa Wahyi iwe Madani.

Jina la Sura linarejelea mngurumo wa mbingu, ambao umetajwa kuwa ni Tasbeeh (Kumtukuza Mwenyezi Mungu) katika aya ya 13 ya sura hiyo: “Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia, kwa kumkhofu. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Mwenye adhabu kali!"

Katika kufasiri Aya hii, wengine wamesema kwamba radi ni ishara ya adhama ya Mwenyezi Mungu na hivyo inawalingania watu kuelekea kwenye Tasbeeh (kumtukuza Mwenyezi Mungu) au radi yenyewe inamtukuza Mwenyezi Mungu. Katika tafsiri nyingine, imesemwa kwamba yeyote anayesikia sauti ya ngurumo, atamtukuza Mungu. Pia kuna dua za kusomwa wakati wa kusikia radi.

Sura hii inazungumzia Tawhid au uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukweli wa Qur'an na Utume wa Mtume wa Mwisho (SAW), Ufufuo, na maelezo ya Pepo na moto. Mada muhimu zilizojadiliwa katika Sura hii ni Tawhiyd, Siku ya Kiyama, na Wahy (Wahyi). Inawaalika wanadamu kutafakari na kutafakari yaliyowapata watu walioishi zamani.

Surah Ar-Ra’ad iliteremshwa kwa kujibu makafiri ambao hawakuitambua Qur'anI kuwa ni muujiza na ishara ya Mwenyezi Mungu na kumtaka Mtukufu Mtume (SAW) awaonyeshe muujiza. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasisitiza katika Sura hii kwamba Qur'ani ni haki, ambayo haijachanganyika na batili.

Sura hii ina moja ya maonyo muhimu zaidi ya Qur'ani kwa wanadamu na jamii za wanadamu. Onyo hilo liko katika aya ya 11: “… Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao...”

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu habadilishi hatima ya watu wowote na wala hawaadhibu isipokuwa washike njia ya uasi  na dhambi. Ni kanuni ya Mwenyezi Mungu kwamba katika jamii yoyote, wakati kutoshukuru na dhambi kutachukua nafasi ya shukrani na kumtii Mwenyezi Mungu, furaha hugeuka kuwa huzuni.

Habari zinazohusiana
captcha