IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /33

Sura Al-Ahzab; Mtazamo sawa wa Qur'ani kuhusu wanaume, wanawake

21:00 - October 02, 2022
Habari ID: 3475870
TEHRAN (IQNA) – Tofauti kati ya wanaume na wanawake ipo tu kwenye miili yao kwani wote wawili kwa mtazamo wa kiroho wako sawa na wanaweza kufikia ukamilifu. Uislamu hauoni tofauti kati ya wanaume na wanawake kwa mtazamo huu.

Surah Al-Ahzab ni sura ya 33 ya Quran Tukufu. Ikiwa na jumla ya aya 73, Sura hiyo ipo katika Juz 21 na 22 ya Kitabu kitukufu. Sura ya Madani, ni Sura ya 90 iliyoteremshwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Jina limechukuliwa kutoka kwa Ghazwat al-Ahzab (Vita vya Makundi) ambayo imerejelewa katika aya za 9-25. Neno "Ahzab" limetajwa katika aya ya 20 na 22 na linaashiria kwa makundi ya makafiri ambao walikuwa wamejenga kiapo cha utii wa kukabiliana na Uislamu na Mtume Muhammad (SAW), kuanzisha vita vya makundi.

Matukio yaliyotajwa katika Sura yalitokea kati ya mwaka wa 2 hadi 5 wa kalenda ya Hijria Qamari. Wakati huo, serikali ya Kiislamu huko Madina ilikuwa katika hatua zake za awali na Waislamu walikuwa wakipitia hali ngumu huku makafiri, Wayahudi, na wanafiki wakiwasumbua. Wakati huo huo, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa akijitahidi kuunganisha kanuni za kijamii na kukabiliana na mila  potovu za Enzi ya Ujahilia  au ujinga kwa upande mmoja, na kupinga juhudi za maadui kwa upande mwingine.

Sura hii ina habari kuhusu nafasi ya wake za Mtume SAW huku pia ikitaja yale yanayotarajiwa kutoka kwao kama vile kupuuza mambo ya kidunia, kushindana na wengine katika kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu, kujiepusha na madhambi, na kutotoka nje ya nyumba.

Miongoni mwa nukta nyingine za Sura ni kwamba inahusu kufanana kati ya wanaume na wanawake katika kupata sifa nzuri. Aya ya 35 ya Sura inasema: “Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.”

Aya hii inataja sifa 10 za hali ya juu kwa wanaume na wanawake wote. Baadhi ya vipengele hivi vinahusiana na imani na vingine vinahusiana na maadili; baadhi ni kuhusu  Wajib (lazima) na vingine ni kuhusu Mustahabb (iliyopendekezwa). Hii inaonyesha kuwa wanaume na wanawake wanafanana katika kufikia sifa hizi zote. Aya hii ni mfano wa mtazamo sawa wa Uislamu kwa wanaume na wanawake.

Habari zinazohusiana
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha