IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /16

Surah An-Nahl: Inaangazia baraka zisizohesabika za Mwenyezi Mungu

12:40 - July 04, 2022
Habari ID: 3475462
TEHRAN (IQNA) – Baraka za Mwenyezi Mungu hazina idadi. Wengine hutafakari juu ya neema au baraka hizo na wengine hawajali au wanapuuza.

Surah An-Nahl ya Qur'ani Tukufu inaorodhesha baadhi ya baraka za Mwenyezi Mungu, ikiwaalika watu kuzitafakari ili waweze kukua kiroho.

Surah An-Nahl ni sura ya 16 ya Qur'ani Tukufu. Ni sura ya Makki, yaani iliyoteremka Makka,  na ni Sura ya 70 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW). Ina Aya 128 na imo katika Juz 14 ya Kitabu kitukufu.

Jina linalojulikana la Surah ni An-Nahl, maana yake nyuki wa asali, kama aya yake ya 68 inavyotaja nyuki wa asali. Sura hii inaangazia baraka na zawadi nyingi za Mwenyezi Mungu na inataja kwa ufupi,  kuhusu maumbile ya kustaajabisha ya nyuki wa asali, ikiashiria badhi ya sifa zake na kumwachia msomaji kugundua baadhi ya nyingine.

Lengo kuu la Sura ni kuangazia baraka za Mwenyezi Mungu, ikiwa ni pamoja na mvua, mwanga wa jua, mimea na matunda mbalimbali, vyakula na wanyama. Hii inalenga kuwaalika watu kwenye shukrani, kutafakari, kunyenyekea kwa amri za Mungu na kukumbuka.

Sehemu nyingine ya Surah An-Nahl inafafanua juu ya kanuni tofauti za Kiislamu kama zile zinazohusiana na Adl (haki), Ihsan (kufanya vitendo vyema), Hijra (kuhama au kugura), Jihad (kupambana kwenye njia ya Mungu), kukataza maovu, dhulma, ukosefu wa haki, uvunjaji wa ahadi, na mwaliko wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi zake. Aya kadhaa za Sura zinamtaja Nabii Ibrahim (AS), bingwa wa Tauhidi, kama mja wa Mwenyezi Mungu mwenye shukrani.

Miongoni mwa sheria za Kiislamu zilizoainishwa katika sura hii ni zile zinazosema kunywa mvinyo na damu na kula nyama ya nguruwe na nyama ya wanyama waliokufa ni haramu.

Pia katika Sura hii imetajwa siku ya Wayahudi ya Jumamosi (Sabato). Katika aya wa 124 tunasoma kwamba: " Hakika siku ya Sabato (Jumaamosi) waliwekewa wale walio khitalifiana kwa ajili yake. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana."

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :