IQNA

Sura za Qur'ani/ 6

Surah Al-An'am: Tamko Kamili la Imani na Sharia ya Uislamu

17:41 - June 07, 2022
Habari ID: 3475347
TEHRAN (IQNA)- Surah An'am inarejelea kisa cha Nabii Ibrahim AS na utume wa watoto wake na inatanguliza dini ya Kiislamu kuwa ni mwendelezo wa njia na malengo ya mitume waliotangulia.

Jina la sura ya sita ya Qur'ani Tukufu ni "An'am" maana yake ng'ombe au mifugo wa miguu minne. Sura hii ina aya 165 ambazo zimejumuishwa katika Juzuu za saba na ya nane.  Surah An'am kwa mpangilio wa wahyi ni sura ya hamsini na tano iliyoteremshwa kwa Mtume Muhammad SAW na ni Makki yaani iliteremka Makka. Katika surah za Makka, kuna maelezo ya kanuni za Imani ya dini, yaani Tauhidi, Unabii na Ufufuo.

Surah An'am ni miongoni mwa Surah ambazo Aya zake zote zimeteremshwa kwa Mtume (SAW) kwa wakati moja. Pia ni mojawapo ya surah za 'Hamidat' kwa sababu inaanza kwa Kumhimidi Mwenyezi Mungu.

Sababu ya kuitaja surah hii kuwa ni "An'am" ni kuzungumzia ng'ombe katika Aya zake kumi na tano. Sura hii inahusu ng'ombe, wanyama wa kufugwa kama ng'ombe, kondoo, ngamia na mbuzi.

Kusudio kuu la surah hii ni kudhihirisha Tauhidi au kuthibitisha Mungu mmoja kwa mwanadamu na walimwengu wote. Kwa ajili hiyo, kisa cha mazungumzo ya Nabii Ibrahim na makafiri kuhusu ubatili wa kuabudu nyota, mwezi na jua kimetajwa katika surah hii. Kufuatia kusimuliwa kwa hadithi hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu anataja kukubaliwa kwa ombi la Nabii Ibrahim AS la utume wa Isaka na Yakub na kizazi kingine chake, na kwa sababu hii, surah hii ina majina 17 ya manabi. Baada ya hapo Qur'ani Tukufu inamtaja Mtume wa Uislamu, Muhammad SAW kama mrithi na wasii wa Mitume hao wote wa Mwenyezi Mungu, na hivyo inabidi atangaze kwamba mwito wake kwa wanadamu kuja katika Uislamu si wa kitaifa au wa kikabila, na kwamba unaelekezwa kwa walimwengu wote.

Surah An'amni tangazo kamili la ya imani na sheria ya Kiislamu. Katika surah hii yote, kauli zake ni jibu la shaka na pingamizi za wapinzani wa Uislamu na Mwenyezi Mungu, ambazo zimeelezwa na Mtume Muhammad SAW kupitia surah hii. Kurudiwa kwa kauli hii "Qul: Maana yake ni "Sema" mara 44 katika surah hii ni ishara ya msisitizo unaofuatana wa kukabiliana na shaka na ni kama hoja dhidi ya washirikina na wapinzani wa Tauhidi, Unabii na Ufufuo. Juhudi za mara kwa mara za Qur'an kusahihisha imani ya mwanadamu, hasa kuhusu Mwenyezi Mungu na ibada, zimeonyeshwa wazi katika surah hii.

Habari zinazohusiana
captcha