IQNA

Sura za Qur'ani/ 8

Sura Al-Anfal; Maelezo kuhusu maana halisi ya Jihad katika Uislamu

23:45 - June 16, 2022
Habari ID: 3475385
TEHRAN (IQNA)- Kuongezeka kwa makundi ya kigaidi duniani na matumizi mabaya ya Uislamu kumepelekea istilahi Jihadi (vita vitakatifu) kupachikwa maana isiyo sahihi na hivyo kunasibishwa na maneno kama vile kuchochea vita, ghasia na mauaji.

Hata hivyo, Uislamu daima unasisitiza amani huku pia ukitilia mkazo kuhusu muhimu wa Jihadi ya kujitetea mbele ya wavamizi.

Al-Anfal ni jina la sura ya 8 ya Qur’ani; Sura hii ya Madani ina aya 75 na iko katika Juzi za 9 na 10 za Qur’ani Tukufu. Anfal maana yake ni nyara na sura imepewa jina ipasavyo kwa sababu aya ya kwanza ina neno hili na inatoa sheria kuhusu kugawanya na kutumia ngawira. sura pia inaelekeza kwenye kanuni za kifiqhi za ngawira na mali ya umma, khums, jihadi, kazi za Mujahidina, jinsi ya kuwatendea wafungwa wa vita, ulazima wa kudumisha utayari wa kijeshi, na dalili za Muumini.

Sura hii imeteremshwa kwa Mtume Muhammad (SAW) baada ya Vita vya Badr. Hii ilikuwa ni Jihadi ya kwanza ya Waislamu na hivyo kumekuwa na haja ya maelekezo kuhusu vita na yale yanayofuata kama vile jinsi ya kuwatendea wafungwa na jinsi ya kugawanya ngawira.

Aya ya 61 ya Sura inasema: Na iwapo wao (makafiri) wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.”

Aya hii, ambayo pia inajulikana kama aya ya amani, inazungumzia juu ya kukubali amani bila ya masharti yoyote mbele ya pendekezo la upande mwingine katika vita na hii inaonyesha umuhimu wa amani katika mafundisho ya Kiislamu.

Aya hii inadhihirisha kwamba Uislamu hautokani na vita, bali unalenga kueneza amani na utulivu. Pamoja na hayo, kuna aya nyingine katika Quran zinazowataka Waislamu kuwa macho endapo adui atatumia njia hii vibaya.

Lengo kuu la sura ni kueleza jinsi waumini wanavyoweza kufaidika na msaada wa Mwenyezi Mungu. Inataja kumtii Mungu na mjumbe wake kama masharti makuu. Sura hiyo pia inasisitiza kwamba Mungu Mwenyezi bila shaka atatimiza ahadi zake.

Kisa cha Mtume Muhammad (SAW) kugura kutoka Makka hadi Madina ni moja ya maudhui nyingine katika sura hii. Katika sura hii, wanaogura (Hijrah) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamepongezwa.

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha