IQNA

Ifahamu Qur'ani Tukufu/19

Qur'ani Tukufu ni ujumbe bora zaidi

22:15 - July 29, 2023
Habari ID: 3477355
TEHRAN (IQNA) - Katika dunia ya leo, mabilioni ya sentensi huchapishwa au kutangazwa na wasemaji na wazungumzaji. Lakini ni maandishi ya Qur'an Tukufu ambayo yana vipengele ambavyo Kitabu kitukufu kinajieleza kama "Ujumbe Bora".

Qur’ani Tukufu inasema katika Aya ya 23 ya Sura Az-Zumar: “ Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.”

Neno la Kiarabu lililotumika katika aya hii ni hadith kwa Qur'ani Tukufu na kishazi ‘Ahsan al-hadith’ (hadithi bora) inasisitiza ukamilifu wa Qur'ani Tukufu, ukweli, uthabiti, na ufasaha.

1- Ukamilifu: Qur'ani Tukufu inajumuisha kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya mwongozo na ukuaji wa wanadamu. Pia, kwa sababu Qur'ani Tukufu ni kitabu cha mwisho cha Mwenyezi Mungu, ina mafundisho na mwongozo uliojumuishwa katika vitabu vyote vilivyotangulia.

2- Ukweli: Kwa kuzingatia Aya ya 81 ya Sura Al-Isra: “Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!” ukweli daima utaushinda uwongo mwishoni. Kwa vile Qur'an ni haki, na ukweli daima ni ushindi, Qur'ani itashinda katika kila pambano na uwongo na hivyo nuru ya Qur'an kamwe haiwezi kuzimwa. " Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia." (Aya ya 8 ya Surah Saff)

3- Uthabiti: Uthabiti wa Quran upo katika ukweli kwamba ni kitabu cha mwisho cha Mwenyezi Mungu. Hakujawa na mabadiliko au upotoshaji ndani yake na hakuna kitabu cha kiungu kitakachoteremshwa baada yake. Hivyo Qur'ani Tukufu itabaki imara na thabiti milele.

4- Ufasaha: Hii inahusu uzuri wa neno la Mungu na kuwa sahili na wakati huo huo ni wa kina. Qur'ani  Tukufu inazungumza na watu kwa namna ambayo kila mtu anaelewa lakini wakati huo huo inafikisha kiwango cha juu cha elimu na hekima.

Neno Mutashabih (sawa) katika Aya hii linasisitiza kwamba sehemu mbalimbali za Qur'ani Tukufu zinapatana na hakuna migongano na kutofautiana ndani yake.

Katika hotuba na maneno ya wanadamu, kuna tofauti na kinzani bila kujali jinsi wanavyojaribu sana kuziepuka.

Katika Quran, kuna mshikamano na mfungamano wa ajabu katika dhana na mafundisho katika aya zote, jambo ambalo ni uthibitisho wa ukweli kwamba si neno la wanadamu.

Neno jengine katika Aya hii ni Mathani, ambalo maana yake ni Aya na maneno ya Qur'ani Tukufu yanaelekezana, yaani yanafasiriana.

captcha