IQNA

Siasa

Ayatullah Khamenei: Marekani ni chimbuko la matatizo ya eneo la Asia Magharibi

18:48 - October 02, 2024
Habari ID: 3479525
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, chimbuko la matatizo ya eneo la Asia Magharibi ni mataifa kama Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazodai kwa uwongo kwamba, zinataka amani na utulivu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo jijini Tehran alipokutana na mamia ya watu wenye vipaji vya elimu hapa nchini na waliong'ara katika mashindano ya olimpiadi na mitihani ya kuingia katika vyuo vikuu na kusisitiza ulazima wa kunufaika na watu wenye vipaji katika sekta mbalimbali na ulazima wa kuandaliwa mazingira ili watu wenye vipawa wawe na taathira katika masuala mbalimbali ya nchi.

Akizungumzia matukio ya Asia Magharibi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, njia pekee ya kumaliza mizozo na vita katika eneo hili ni kupunguza maovu ya nchi hizi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuchukulia uchochezi wa Saddam wa kuishambulia Iran na siku za machungu na magumu kuwa ni mfano wa wazi wa uanzishaji vita wa Marekani na Magharibi katika eneo na kuongeza: Huba na upendo uliopo hivi sasa kati ya nchi mbili za Iran na Iraq, ambao kilele chake ni katika matembezi makubwa ya Arubaini ya Imamu Hussein (as) ni mfano wa wazi unaoonyesha kuwa sababu kuu ya matatizo ya eneo hili ni wadai bandia wa amani, ambao kkwa tawfiq ya Mwenyezi Mungu na juhudi kubwa za taifa la Iran na kwa msaada wa miongozo ya Mapinduzi ya Kiislamu na ushirikiano wa mataifa mengine maovu yao yatapungua katika eneo.

"Nina maoni kuhusiana na masuala ya Lebanon na mambo yanayohusiana na shahidi huyu mkubwa na mpendwa, ambayo nitayataja katika siku za usoni, Mungu akipenda," Ayatollah Khamenei alisema, akimzungumzia Sayed Hassan Nasrallah, katibu mkuu wa Hizbullah, ambaye aliuawa siku ya Ijumaa katika shambulizi la kigaidi la Israel huko Beirut. Aidha Kiongozi Muadhamu amesema atazungumza kuhusu Ukanda wa Gaza hivi karibuni.

Mkutano huo wa Kiongozi Muadhamu na wasomi unakuja siku moja baada ya jeshi la Iran kutekeleza operesheni ya 'Ahadi ya Kweli II', inayolenga ngome za kijeshi na usalama za Israel kujibu mauaji ya Israel ya mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas Ismail Haniya, kiongozi wa Hizbullah Hassan Nasrallah, na kamanda mwandamizi wa IRGC Abbas Nilforoushan.

4240134

Habari zinazohusiana
captcha