IQNA

Muqawama

Ayatullah Khamenei: Utawala wa Kizayuni umejiandalia uwanja wa kuadhibiwa vikali

20:08 - July 31, 2024
Habari ID: 3479207
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe maalumu baada ya kuuawa shahidi Ismail Haniya Mkuu wa Tawi la Kisiasa la HAMAS akisisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umejiandalia uwanja wa kuadhibiwa vikali.

Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Ayyatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumatano ametoa ujumbe akisisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni ambao ni mtenda jinai na ni utawala wa kigaidi, umemuua shahidi mgeni wetu kipenzi kwenye nyumba yetu na kututia majonzi makubwa, hivyo utawala huo umejiandalia mazingira ya kuadhibiwa vikali.

Katika ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, shahid Ismail Haniya ametumia miaka mingi ya umri wake kuendesha mapambano ya kishujaa na kujitolea muhanga roho yake katika njia ya haki na muda wote alikuwa tayari kwa ajili ya kufa shahidi katika mapambano hayo. Ametoa muhanga pia wanawe na watu wake wa karibu katika njia hiyo. Haniyeh amekufa shahidi katika njia ya Allah na kwa ajili ya kuwaokoa waja wa Mwenyezi Mungu. Lakini sisi kuhusu tukio hilo chungu na zito ambalo limefanyika ndani ya mipaka ya Jamhhuri ya Kiislamu, tunasema kwamba kulipiza kisasi damu yake ni jukumu na wajibu wetu. 

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Ismail Haniyeh; kwa Umma wa Kiislamu, kwa Kambi ya Muqawama na kwa taifa shujaa la Palestina hususan watu wa familia ya shahid huyo pamoja na mlinzi wake na amewaombea dua za kupandishwa daraja za juu mbele ya Mola Mtukufu.

Ofisi ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) mapema leo asubuhi imetangaza kuwa, Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS na mlinzi wake mmoja, saa nane za usiku wa kuamkia leo Jumatano, Julai 31, 2024 kwa majira ya Tehran, wameuawa shahidi kwa kupigwa na kitu katika nyumba waliyokuwa wamefikia hapa Tehran kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za kuapishwa Rais wa 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

3489319

Habari zinazohusiana
captcha