IQNA

Mauaji Gaza: Shambulio la Israel laua watu 100 wakiwemo watoto wengi

14:33 - April 04, 2025
Habari ID: 3480492
IQNA – Mashambulizi ya anga ya utawala katili wa Israel katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100, wakiwemo 33 waliokuwa wakijisitiri katika shule.

Maafisa wa Afya wa Gaza wameripoti kuwa mashambulizi hayo ya Alhamisi yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 100, wakiwemo angalau 33 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika shule iliyoko mtaa wa Tuffah, katika mji wa Gaza.

Zaher al-Wahidi, msemaji wa Wizara ya Afya, alithibitisha kwamba miili ya watoto 14 na wanawake watano imepatikana kutoka katika shule hiyo, huku akionya kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwani baadhi ya majeruhi 70 wamo katika hali mahututi.

Zaidi ya watu 30 pia walipoteza maisha yao katika mashambulizi dhidi ya nyumba za makazi katika eneo la Shijaiyah, jirani na hapo, kwa mujibu wa hospitali ya Ahli.

Siku moja kabla ya tukio hilo, kituo cha hifadhi cha Umoja wa Mataifa kilishambuliwa, na kusababisha vifo vya angalau watu 17, hali iliyoongeza ukali wa mgogoro huo.

Wakati huo huo, wanajeshi wa Israel wamepanua kile wanachokiita eneo la usalama kaskazini mwa Gaza, na kulazimisha mamia ya wakaazi kuhama kwa miguu, baiskeli, magari madogo au mikokoteni ya punda.

Katika hali hii ya hatari, rais wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina, Younis Al-Khatib, ametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu uhalifu wa Israel na kuwawajibisha wahusika.

Al-Khatib alionya kuwa mfumo wa misaada ya kibinadamu Gaza uko hatarini kuporomoka. Alisema Hilali Nyekundu imepoteza wafanyakazi 30, wakiwemo wanane waliouawa Tel al-Sultan, Rafah, ambapo mfanyakazi mmoja bado hajapatikana.

Shirika hilo limeitaka Israel kutoa taarifa juu ya wafanyakazi wao waliopotea na kuongeza ulinzi kwa wahudumu wa misaada.

Mapema siku ya Alhamisi, Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza ilisema kuwa watu 1,163 wameuawa katika eneo hilo tangu Israel ilipovunja mapatano ya usitishaji vita tarehe 18 Machi baada ya kusitishwa kwa vita kwa muda wa wiki sita.

Zaidi ya Wapalestina 50,500 wameuawa kaktika mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekelezwa na utawala haramu wa Israel huko Gaza tangu Oktoba 2023, na angalau 114,000 wamejeruhiwa.

3492562

Habari zinazohusiana
captcha