IQNA

Mtoto wa Malaysia wa miaka 10 afanikiwa kama Muadhini licha ya ulemavu wa macho

19:13 - April 01, 2025
Habari ID: 3480482
IQNA – Licha ya ulemavu wa machi, Muhammad Hafizuddin Muhammad Amirul Hakim Linges mwenye umri wa miaka 10 ana uwezo wa kipekee.

Tangu akiwa na umri wa mwaka mmoja, alionyesha kuvutiwa sana na masuala ya Uislamu. Kufikia umri wa miaka minne, alikuwa ameanza kuhifadhi Surah Yasin, na kufikia miaka sita, alikuwa ameihifadhi kikamilifu. 

Baadaye aliendelea kuhifadhi surah zingine muhimu, ikiwemo Al-Mulk, Al-Kahfi, Ar-Rahman, As-Sajdah, Al-Insan, Juz Amma, na aya 101 za kwanza za Surah Al-Baqarah. 

Upendo wake kwa msikiti unaonekana katika ushiriki wake wa karibu kwenye karibu shughuli zote zinazofanyika hapo, jambo ambalo lilimfanya apewe imani ya kutumikia kama ‘Bilal Mtoto’ katika Msikiti wa At-Taqwa, Taman Tun Sardon, karibu na Gelugor nchini Malaysia. 

Hata akiwa mdogo sana, anaonyesha ukomavu unaozidi umri wake. Sauti yake nzuri, haswa anaposoma aya za Qur’ani na kuadhini, inamfanya awe mtoto wa kipekee. 

Mama yake, Wan Dalila Diyana Wan Mustoffa, mwenye miaka 42, amesema kwamba Muhammad Hafizuddin hakuwahi kumjua baba yake, ambaye alifariki kutokana na saratani ya ubongo wakati alikuwa na mimba ya miezi saba. 

Kwa kusikitisha, akiwa na umri wa miezi minne tu, Muhammad Hafizuddin aligundulika na saratani ya macho, ambayo ilimwacha akiwa kipofu kwa jicho lake la kushoto na kupungukiwa uwezo wa kuona katika jicho lake la kulia. 

Wan Dalila, ambaye pia ana upungufu wa uwezo wa kuona, aligundua mapema upendo wa mwanawe kwa dini alipokuwa na umri wa mwaka mmoja, kwani angemwomba aswali mara baada ya kusikia adhan kutoka msikiti wa karibu. 

"Kila baada ya adhana, alikuwa na hamu ya kutuhimiza kwenda msikitini. Amekuwa akiswali hapo tangu akiwa na miaka mitatu, mara nyingi akiwa na babu yake. 

"Msikiti ni kama nyumba yake ya pili, ambapo hutumia muda wake mwingi," alisema, akiongeza kwamba Muhammad anapenda kusoma dhikr na salawat, pamoja na kuhudhuria madarasa ya kuhifadhi Qur’ani. 

"Zawadi yake iko katika uwezo wake wa kumsikiliza imam na kuhifadhi peke yake. Mimi husaidia tu kumwelekeza na kumrekebisha ikiwa amekosea harufu au nukta kutokana na kasi yake. Hata shuleni, walimu wake walitambua uwezo wake alipokuwa na miaka sita na kumwamini aongoze swala na dua," alisema kwenye mahojiano na Bernama hivi karibuni. 

Wan Dalila anaona uwezo wa mwanawe kama baraka ya Mwenyezi Mungu. Anaomba imani yake iwe thabiti, moyo wake uangaze kwa kuhifadhi Qur’ani, na apewe husnul khatimah (kifo kizuri). Tamanio lake kubwa ni kumwona akiwa amehifadhi Qur’ani Tukufu kikamilifu siku moja. 

Kwa upande wake, Muhammad Hafizuddin alieleza upendo wake wa kusikiliza qiraa ya imam wakati wa swala na kutamani kuwa imam au muadhini. 

Anatarajia pia kujiunga na shule ya tahfidh na hatimaye kutimiza ndoto yake ya kuwa Hafidh. 

"Ninashukuru na ninafurahi kuwa bilal hapa. Inshallah, siku moja nataka kuwa imam au Bilal (Muadhini). Ninalenga kuhifadhi angalau nusu ya Qur’ani kufikia wakati nitakapokuwa na miaka 12, kabla ya kwenda shule ya tahfidh," alisema mwanafunzi wa Madrasah Uthmaniah (ABIM) Sungai Ara. 

Muhammad Hafizuddin amefafanua kuhusu mbinu yake ya kuhifadhi, akieleza kuwa anasoma aya mara saba, kisha kufunga Qur’an na kuisoma kwa kukariri mara tatu. 

Anaanza siku yake saa 11 asubuhi, akirekebisha kuhifadhi kwake kabla ya kuswali Subuh, na anaendelea kusoma Qur’ani kabla ya kwenda shule. 

Mweka hazina wa Msikiti wa At-Taqwa, Abdul Aziz Md Noohu, alisema msikiti huo unazingatia kuteua Muhammad Hafizuddin kama nembo ya vijana ili kuhamasisha watoto wengine kushiriki kikamilifu katika shughuli za msikiti. 

"Tunajivunia mafanikio yake na mchango wake licha ya kuwa na umri wa miaka 10 pekee. Tumeandaa programu nyingi za kukuza vipaji vya vijana katika jamii yetu, tukiwaandaa kuwa Bilal na imam wa siku za usoni. 

"Tumempa fursa ya kuadhini, na Ramadhani hii, alialikwa kutumikia kama Muadhini wakati Sala za Tarawih katika siku 15 za kwanza," alisema. 

3492541

captcha