IQNA

Msomi: Hija Ni Fursa ya Kujitambua

15:44 - May 05, 2025
Habari ID: 3480639
IQNA – Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Hija aameitaja safari ya Hija kama fursa ya dhahabu ya kujitambua na kupata uelewa wa kina zaidi wa Uislamu.

Hujjatul Islam Seyed Abdol Fattah Navab ameyasema hayo katika sherehe ya kuaga kundi la kwanza la Wairani wanaoelekea katika ibada ya Hija nchini Saudi Arabia.
Hafla hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran siku ya Jumatatu.

Akirejelea msisitizo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyed Ali Khamenei, wakati wa kikao na maafisa wa Hija siku moja kabla kuhusu umuhimu wa kuelewa na kuthamini Hija na kuzingatia uwezo wake wa kiroho, Hujjatul Islam Navab alinukuu riwaya na hadithi kutoka kwa Maimamu (AS) wasiokosea kuhusu elimu na maarifa katika dini.

Alieleza kwamba Imam Ali (AS) alisema hakuna tendo au shughuli yoyote isiyohitaji maarifa kuhusu yenyewe, na kwa hivyo aliwasihi Mahujaji wote wazingatie kwa makini uelewa wa kiroho wa ibada za Hija na kutumia huduma za maulamaa walioko katika misafara ya Hija, ambao wako tayari kuwahudumia Mahujaji masaa 24.

Kujitambua katika dini kunashikilia nafasi ya pekee sana, hata muhimu zaidi kuliko maarifa ya desturi za ibada, kwa sababu kupitia kujitambua mtu pia anaweza kupiga hatua katika kuelewa mafundisho ya imani, alibainisha.

Aliyataja mahesabu ya nafsi na kujitathmini kama masharti muhimu ya marekebisho ya binafsi na kusema kwamba siku za Hija zinatoa fursa ya msingi na adimu ya kutafakari, kujitambua, na kutubu. 

Takribani Wairani 85,000 wanatarajiwa kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Hija ni safari takatifu kuelekea mji mtukufu wa Makka ambayo kila Mwislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha analazimika kuitekeleza angalau mara moja maishani mwake. 

Hija hii ya kila mwaka inachukuliwa kama moja ya nguzo za Uislamu na ndiyo ibada kubwa zaidi ya pamoja duniani. Pia ni ishara ya umoja wa Waislamu na unyenyekevu wao kwa Mwenyezi Mungu.

3492945

Kishikizo: hija iran
captcha