IQNA

Hija 1445

Zaidi ya Wairani 45,500 tayari wamefika Saudia kwa ajili ya Hija

18:40 - May 31, 2024
Habari ID: 3478905
IQNA - Zaidi ya nusu ya Wairani wanaotarajiwa kuhiji mwaka huu wamewasili Saudi Arabia, afisa mmoja alisema.

Gholam Reza Rezaei, Mkurugenzi wa Operesheni za Hija katika Shirika la Hija la Iran alisema siku ya Alkhamisi kwamba Wairani 45,553 wamewasili katika miji mitakatifu ya Makka na Madina kufikia Jumatano usiku.

Hii inachangia takriban asilimia 53 ya Wairani waliojisajili kushiriki katika ibada ya Hija mwaka huu wa 1445 Hijria Qamaria sawa na  2024, alibainisha.

Rezaei ameongeza kuwa, Wairani wengi wanaosafiri kuelekea nchi hiyo ya Kiarabu kwa ajili ya Hija hadi sasa wameingia nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Madina.

Wengine hadi sasa wamesafiri au watasafiri hadi Saudi Arabia katika siku zijazo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jeddah, alisema.

Hija ni safari ya kwenda Makka ambayo kila Mwislamu mwenye uwezo wa kimwili na uwezo wa kifedha anapaswa kutekeleza  angalau mara moja katika maisha yake.

Hija ya kila mwaka inachukuliwa kuwa moja ya nguzo za Uislamu na ni mjumuiko mkubwa zaidi wa aina yake dunia kwani waumini karibu milioni 2.5 hukusanyika katika eneo moja katika siku maalumu na kutekeleza ibada zote kwa pamoja. Hija ni  dhihirisho la umoja wa Waislamu na kunyenyekea kwao kwa Mwenyei Mungu.

3488564

Kishikizo: hija iran
captcha