IQNA

Kundi la kwanza la Mahujaji kutoka Iran kuelekea Saudia Juni 13

18:50 - May 06, 2022
Habari ID: 3475214
TEHRAN (IQNA)- Ndege ya kwanza itakayokuwa imewabeba watu wa Iran wanaokusudia kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu itaondoka Tehran kuelekea Saudia mnamo Juni 13.

Hayo yamedokezwa na Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Abdul Fattah Navab Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu katika masuala ya Hija na Ziara.

Aliyasema hayo jana baada ya kuonana na Maayatullah Naser Makarim Shirazi, Hossein Nour Hamedani na Jafar Sobahani katika mji mtukufu wa Qum na kuongeza kuwa, mwaka huu mahujaji 39,600 wa Iran watakwenda kutekeleza ibada ya Hija katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina.

Mwakilishi huyo wa Kiongozi Mkuu wa kidini nchini Iran amegusia pia masharti yaliyowekwa na Saudi Arabia ya kuitaka Iran ipelekea asilimia 45 tu ya mahujaji mwaka huu tena walio na umri wa chini ya miaka 65 na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tayari imeiandikia barua serikali ya Saudi Arabia na kuipa mapendekezo yake kuhusu kuongezwa idadi ya mahujaji wa Iran na kupandishwa pia umri wa mahujaji yaani kuruhusiwa kuhiji hata walio na zaidi ya miaka 65 akisema kuwa, ana matumaini mamlaka za Saudia zitazingatia mapendekezo hayo ya Iran.

Kwa upande wake, Sayyid Sadeq Hosseini, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ndege ya kwanza ya mahujaji itaelekea nchini Saudi Arabia kutokea Iran tarehe 13 Juni mwaka huu wa 2022 na ndege ya mwisho kuelekea nchini humo kwa ajili ya ibada ya Hija itasafiri tarehe 28 mwezi huo wa Juni tukijaaliwa.

Mahujaji hao wote ni wale waliotimiza masharti yakiwemo ya kupiga chanjo kamili za kujikinga na ugonjwa hatari wa corona.

Hivi sasa kuna Wairani milioni 5.8 ambao wamejiandikisha kutekeleza ibada ya Hija na Umrah nchini Saudia na wangali wanasubiri zamu yao.

4054904

Kishikizo: hija saudia iran
captcha