IQNA

Msomi wa Kiislamu akanusha madai kuwa Mashia wamejitenga na Qur'ani

17:38 - May 19, 2025
Habari ID: 3480707
IQNA – Mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Iran amepinga madai kwamba Waislamu wa madhehebu ya Shia hawana uhusiano wa karibu na Qur'ani Tukufu huku akiyataja madai kama hayo kuwa ni uzushi wa muda mrefu unaoenezwa na maadui wa Uislamu.

Hujjatul-Islam Seyyed Abdolfattah Navvab, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya Hija ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Hija wa Iran, amekanusha dhana potofu kwamba Uislamu wa Kishia hauna uhusiano wa karibu na Qur'ani Tukufu.

Akizungumza siku ya Jumapili, Mei 19, katika mkutano na wanachama wa Msafara wa Nur wa Qur'an huko Madinah, Hujjatul-Islam Navvab alisema: "Maadui wamejaribu kuonyesha Mashia kuwa wanashikamana tu na Ahl al-Bayt (AS) bila kuwa na uhusiano na Qur'ani. Lakini mwenendo wa Ahl al-Bayt (AS), mafundisho ya wanazuoni wa Kishia, na upeo wa Imam Khomeini (MA) pamoja na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu vimebatilisha propaganda hii."  

Hujjatul-Islam Navvab alitoa mifano ya kihistoria kuonyesha heshima ya kina kwa Qur'anI ndani ya mila za Mashia. "Chukua mfano wa Fizza, mtumishi wa Bibi Fatima Zahra (SA), ambaye alijulikana kwa kuzungumza kwa kutumia aya za Qur'ani pekee kwa zaidi ya miongo miwili. Au fikiria mfano wa hivi karibuni—wakati kijana wa Kiirani, Seyyed Mohammad Hossein Tabatabai, aliyehifadhi Qur'ani, alipotembelea Saudi Arabia, alijibu maswali yote kwa kutumia marejeo ya Qur'ani, jambo lililowashangaza maafisa wengi waliokuwepo."

Akisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano wa kudumu na Qur'ani, aliongeza: "Njia za ubunifu zinahitajika ili kuimarisha uhusiano huu; ingawa ukubwa wa hadhira ni muhimu, lengo halisi linapaswa kuwa ubora na athari za programu za Qur'ani."

Msafara wa Nur wa Qurani, ambao Hujjatul-Islam Navvab alikutana nao, ni sehemu ya juhudi pana za Iran za kuimarisha tajiriba ya kiroho ya Mahujaji kwa kuandaa matukio yanayohusiana na Qur'anI wakati wa Hija.

Kila mwaka katika fremu ya Msafara wa Nur wa Qur'ani, Iran hutuma timu ya maqari na wahifadhi wa Qur'ani kuandamana na mahujaji kuelekea Makkah na Madinah.

Katika msimu wa Hija mwaka huu, msafara huu unajumuisha wanachama 20—maqari 14, mmoja aliyehifadhi Qur'ani kikamilifu, na kikundi cha watu watano cha Tawasheeh (nyimbo za kidini). Wamepangiwa kushiriki zaidi ya vikao 220 vya Qur'ani katika kipindi chote cha Hija katika miji mitakatifu.

Hujjatul-Islam Navvab pia amewahimiza wanachama wa msafara huo kueneza maadili ya Kiislamu kupitia usomaji wao wa Qur'ani. "Katika Madinah, maqari wanapaswa kusisitiza maadili na tabia ya Mtume Muhammad (SAW). Aya moja tu, ikitafakariwa, inaweza kubadilisha maisha ya mtu," alisema. "Katika Makkah, msisitizo unapaswa kuwa juu ya urithi wa Mtume Ibrahim (AS), mwanzilishi wa Kaaba."

3493140

Habari zinazohusiana
Kishikizo: hija iran msafara wa nur
captcha