IQNA

Watu wa Gaza waswali Swala ya Idul Adha juu ya magofu ya misikiti

10:38 - June 07, 2025
Habari ID: 3480799
IQNA – Wapalestina kote Ukanda wa Gaza wameswali Swala ya Idul Adha juu ya magofu ya misikiti iliyoharibiwa na vita vya kinyama vya utawala wa Israel dhidi ya eneo hilo.

Wapalestina wameadhimisha Sikukuu hiyo Ijumaa, wakiwa na matumaini haba kuwa vita dhidi ya Israel vitakoma hivi karibuni.

Katika maeneo mengi ya Gaza yaliyogeuzwa kuwa kifusi, wanaume na watoto walilazimika kuswali Idi wakiwa nje, huku uhaba mkubwa wa chakula ukilazimisha familia kujikusanya na kula chochote walichoweza kupata kwa ajili ya sherehe za siku tatu za Idi.

“Hii ndiyo Idi mbaya zaidi ambayo watu wa Palestina wamewahi kushuhudia kutokana na vita hivi vya dhuluma dhidi ya wananchi wa Palestina,” alisema Kamel Emran baada ya kusali katika mji wa Khan Younis ulioko kusini mwa Gaza.

“Hakuna chakula, hakuna unga, hakuna makazi, hakuna misikiti, hakuna nyumba, hata magodoro hakuna… Hali ni ngumu mno.”

Sikukuu ya Kiislamu ya Idul Adha huanza siku ya 10 ya mwezi wa Dhul-Hijja katika kalenda ya Kiislamu, na huambatana na msimu wa Hija huko Saudi Arabia.

Katika Gaza Kaskazini siku ya Ijumaa, Israel ilitoa onyo jipya kwa raia, ikisema jeshi lake lilikuwa linajiandaa kuendesha mashambulizi makali katika eneo moja baada ya kudai kwamba makombora yalirushwa kuelekea maeneo ya Palestina yaliyochukuliwa kwa nguvu.

Tangu Oktoba 7, 2023, utawala wa Israel umewaua zaidi ya Wapalestina 54,500 katika  vita vya mauaji ya kimbari, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.

Mashambulizi hayo yameharibu sehemu kubwa ya Gaza na kuwalazimisha karibu asilimia 90 ya watu wake milioni mbili kuyakimbia makazi yao.

Baada ya kuzuia chakula na misaada yote kuingia Gaza kwa zaidi ya miezi miwili, Israel ilianza kuruhusu misaada michache kupenya kwa ajili ya Umoja wa Mataifa wiki chache zilizopita.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema umeshindwa kusambaza misaada hiyo kikamilifu kutokana na vizuizi vya kijeshi vya Israel juu ya harakati za misaada hiyo.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), lenye makao yake Roma, lilisema Alhamisi kuwa watu wa Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa kali ifikapo Septemba, ambapo karibu watu 500,000 wanakumbwa na upungufu mkubwa wa chakula, hali inayoweza kusababisha utapiamlo na vifo vya njaa.

“Hii ina maana kuwa hatari ya njaa sasa inatishia Ukanda mzima wa Gaza,” alisema Rein Paulson, mkurugenzi wa ofisi ya dharura na uhimilivu ya FAO, katika mahojiano.

 3493344

Habari zinazohusiana
captcha