IQNA

Maelfu washiriki Swala ya Iddi eneo la Bain-ul-Haramain, Karbala, Iraq

16:36 - June 07, 2025
Habari ID: 3480802
IQNA – Maelfu ya wafanyaziara na wakazi wa Karbala walikusanyika kwa wingi kushiriki Swala ya Iddi ul Adha iliyoswaliwa Jumamosi katika eneo la Bain-ul-Haramain.

Bain-ul-Haramain ni eneo tukufu linalotenganisha makaburi ya Imam Hussein (AS) na Hadhrat Abbas (AS) huko Karbala, Iraq , mahali panapobeba uzito mkubwa wa kihistoria na kidini kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Swala hiyo ya Iddi iliongozwa na Sheikh Salah al-Karbalayi, mkuu wa kitengo cha mambo ya kidini katika Idara ya Mfawidhi wa Haram ya Hadhrat Abbas (AS).

Ijumaa jioni, misikiti na vituo vya Kishia kote Iraq vilitangaza kuwasili kwa Idul Adha kwa kutamka kauli mashuhuri: "Allahu Akbar" (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa), kwa mujibu wa desturi za kale, ili kuwawezesha waumini kushiriki katika swala ya Iddi mapema asubuhi ya Jumamosi.

Karbala, ambayo siku ya Ijumaa ilijaa wafanyaziara kutoka Iran na Waislamu wa Iraq waliokusanyika kusoma dua ya Arafah, ilishuhudia pia msongamano mkubwa wa magari yaliyoleta watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya Swala ya Iddi katika Bain-ul-Haramain.

Idul al-Adha ni miongoni mwa sikukuu tukufu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, yenye mizizi katika tukio la kiroho lenye uzito mkubwa lililotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu.

Sikukuu hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 10 ya mwezi wa Dhul Hijjah, mwezi wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu ya Hijria,  ikiwa ni kumbukumbu ya utiifu na unyenyekevu wa Mtume Ibrahim (amani iwe juu yake) na mwanawe Ismail (amani iwe juu yake), walipoitikia amri ya Mwenyezi Mungu kwa moyo wa imani na kujisalimisha.

Kwa mujibu wa mapokezi ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Ibrahim amtoe mwanawe Ismail dhabihu, mtoto aliyemruzuku uzeeni. Bila kusita, baba na mwana walijiandaa kutekeleza amri ya Mola wao kwa moyo wa subira na yakini.

Hata hivyo, wakati Ibrahim alipokuwa karibu kutekeleza agizo hilo, Mwenyezi Mungu alimtuma Malaika Jibril (amani juu yake) na akamletea kondoo wa kuchinjwa badala ya Ismail. Tukio hili limeelezewa kwa uzito mkubwa katika Qur’ani, katika Surah As-Saaffat, aya 106 hadi 109:

“Hakika huu ulikuwa ni mtihani wa dhahiri. Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. Nasi tukamuachia (sifa njema) kwa waliokuja baadaye. Amani iwe juu ya Ibrahim.”

3493353

Kishikizo: idul adha
captcha