Ghorbani alitoa taarifa hiyo Jumatano katika kikao maalum cha maandalizi ya operesheni ya Arbaeen kilichofanyika jijini Tehran.
Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia kipindi cha kilele cha kurejea kwa wafanyaziara, ambacho ni kuanzia jioni ya siku ya Arbaeen hadi siku tatu baada yake.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika, inakadiriwa kuwa mwaka huu wakati wa Arbaeen watu takribani 900,000 wanasafiri kwa basi, milioni 2.4 kwa magari binafsi, 296,000 kwa njia ya anga na 356,000 kwa treni.
Aidha, usafiri wa baharini pia umepangwa ili kuwahudumia wafanyaziara kutoka bandari ya Khorramshahr (Iran) hadi bandari ya Basra (Iraq), aliongeza Ghorbani.
Afisa huyo pia alieleza kuwa asilimia 60 ya wafanyaziara wa Iran watatumia kivuko cha mpakani cha Mehran wakati wa kuelekea Karbala, na asilimia 70 watakitumia wakati wa kurudi.
Kwa mujibu wa maelezo yake, jumla ya mabasi 7,700 yanahitajika kila siku katika siku za kilele za msimu wa Arbaeen. Hata hivyo, kutokana na uwepo wa mabasi 6,500 kwa sasa, hatua maalum zitachukuliwa ili kuongeza idadi inayohitajika.
Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu hasa wa madhehebu ya Shia, siku ya arobaini baada ya siku ya Ashura, ikiwa ni kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imamu wa tatu katika itikadi ya Kishia.
Ni moja ya ziara kubwa kubwa zaidi ya kidini duniani inayofanyika kila mwaka, ambapo mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na baadhi ya Waislamu wa Sunni na hata wafuasi wa dini nyingine, hutembea kwa miguu kuelekea mji mtakatifu wa Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani.
Mwaka huu, siku ya Arbaeen itasadifiana na tarehe 14 Agosti 2025.
3493784