Aref amefanya mazungumzo ya simu nyakati tofauti na waziri wa afya, magavana wa majimbo ya Ilam, Kermanshah, na Khuzestan na mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Alhamisi.
Katika mazungumzo hayo ya simu, alishukuru juhudi zilizofanywa hadi sasa za kuwahudumia wafanyaziayra ya Arbaeen, kuhakikisha usalama na ustawi wao.
Alisema vyombo vinavyohusika vinapaswa kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha kuwa wafanyaziara wanapita vizuri kutoka kwenye mpaka wakati wa kuondoka kuelekea Iraq na kurejea nyumbani.
Aref pia alisisitiza kutumika vifaa na wafanyakazi wote kutoa huduma zote za afya na matibabu kwa wafanyaziara wa Arbaeen.
Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.
Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.
Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.
3489521