IQNA

Wahudumu wa afya Waislamu Australia wakumbwa na ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu

10:24 - July 11, 2025
Habari ID: 3480925
IQNA – Utafiti mpya umeonesha ongezeko la chuki na chuki dhidi Uislamu (Islamofobia) dhidi ya wahudumu wa afya Waislamu nchini Australia, hali inayowaathiri kisaikolojia kwa kiwango kikubwa.

Dkt. Noor Suhana Mohd bado anakumbuka hofu aliyohisi alipodhalilishwa kwa maneno na mgonjwa wakati wa kikao cha tiba. “Alisema, ‘Sihitaji kusikiliza Mwislamu,’” alisimulia katika mahojiano na kituo cha ABC. “Niliogopa. Sikuwa na hakika kama atafanya kitu kibaya zaidi.”

Tukio hilo lilitokea katika mwaka wake wa kwanza akiwa daktari wa familia. Ingawa ni tukio la karibu muongo mmoja uliopita, anasema liligonga imani yake ya kitaaluma na linaendelea kuathiri afya yake ya kiakili hadi leo.

Kisa cha Dkt. Mohd si cha kipekee. Utafiti wa kitaifa uliofanyika mwaka 2024, uliofanywa na ushirikiano wa vyuo vikuu vya Australia na Chama cha Madaktari Waislamu Australia (AIMA), uliwahusisha wahudumu wa afya 358,  asilimia 85 wakiwa Waislamu, wengi wao wakitokea jamii zenye tamaduni na lugha tofauti (CALD).

Matokeo yamebainisha kuwepo kwa unyanyasaji mkubwa wa kidini na wa rangi katika mazingira ya tiba.

“Utafiti huu unaonesha wazi kwamba chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi vinaathiri wahudumu wa afya bila kujali imani au asili yao,” alisema Profesa Muhammad Aziz Rahman wa Chuo Kikuu cha Federation nchini Australia. “Lakini Waislamu , hasa kutoka jamii za CALD , ndiyo wanaoathirika zaidi, na afya yao ya kiakili ipo hatarini.”

Utafiti pia ulibaini kuwa wanawake Waislamu wanakumbwa na “viwango vya juu vya ubaguzi vinavyohusiana na jinsia, utambulisho wa kidini, na muonekano wao wa nje.”

Dkt. Mohd, ambaye kwa sasa ni makamu wa rais wa Chama cha Madaktari Waislamu Australia, alisema matokeo ya utafiti huo yanaonyesha tatizo la kina: “Ninakumbwa na mitazamo ya upendeleo kuhusu uwezo wangu wa kitaaluma na haki yangu ya kuwa chumbani katika mazingira ya matibabu.”

Chama hicho kilionya kuwa hali ya kudumu ya ubaguzi inaweza kusababisha wataalamu Waislamu kujiondoa kazini, hususan katika maeneo ya mbali ambayo tayari yanakosa wahudumu wa afya. 

“Tukiwapoteza wataalamu hawa mahiri kutokana na uchovu wa kiakili au kukata tamaa, wagonjwa wa jamii za pembezoni ndiyo watakaoathirika zaidi,” alisema Dkt. Justin Brown, mtaalamu wa watoto katika masuala ya homoni.

Ripoti hiyo inatoa wito wa maboresho ya haraka ya kimfumo, pamoja na kuwepo kwa msaada wa afya ya akili kwa wahudumu wa afya waliokumbwa na madhila haya.

3493791

captcha