Kwa mujibu wa tovuti ya al-Masrawy, mama huyo aliyefahamika kwa jina la Fatima Ali Muhammad, alikuwa amenyimwa fursa ya elimu tangu utotoni. Lakini kwa azma yake thabiti na msaada wa mjukuu wake, aliweza kuushinda ujinga wa kutokujua kusoma na hatimaye kusoma Qur’ani Tukufu.
Fatima alishiriki mradi wa “Kwa Mshikamano, Hapana kwa Ujinga,” ulioratibiwa na Wizara ya Mshikamano wa Kijamii ya Misri, ambapo alifaulu mtihani wa maarifa ya kusoma na kuandika na kutimiza ndoto yake ya muda mrefu.
Mjukuu wake Alaa Essam anaeleza kuwa bibi yake alipoteza baba akiwa bado mdogo, jambo lililomzuia kuendeleza masomo yake. Alilazimika kuacha shule kabla ya kuhitimu darasa la pili, na nduguze wakawa wakimlea kama mtoto wa mwisho katika familia. Aliolewa akiwa bado mchanga na kujaliwa watoto tisa—watano wa kiume na wanne wa kike.
Licha ya changamoto zake, Fatima alitamani kwa dhati kuona watoto wake wakipata elimu bora, ili wasirudie hali aliyopitia yeye. Matokeo yake, binti zake watatu walihitimu katika vyuo vya ualimu na wote wanahudumu katika shule mbalimbali. Wanawe pia walihitimu elimu ya sekondari na kupata stashahada za biashara na ufundi.
Baada ya kushiriki katika darasa la kuelimisha watu wazima, Fatima alikumbuka ndoto yake ya kusoma Qur’ani Tukufu. Mjukuu wake Alaa alianza kumfundisha herufi na maneno rahisi, kabla ya kumpeleka katika darasa la pili. Hatua kwa hatua, ndoto yake ya kujifunza kusoma ikawa karibu kutimia. Na hatimaye, alifaulu kwa mafanikio makubwa mtihani wa kusoma.
Alaa alieleza furaha yake kwa mafanikio hayo, akisema ameweza kulipa juhudi za bibi yake kwa kumkomboa kutoka ujinga na kutimiza ndoto yake ya kusoma Qur’ani Tukufu.
3493985