IQNA

Harakati ya Qur'ani

Tarjuma ya Kiebrania ya Juzuu 20 za Qur'ani Tukufu yakamilika Misri

19:17 - November 22, 2022
Habari ID: 3476130
TEHRAN (IQNA) – Kazi ya kutayarisha tarjuma ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kiebrania inaendelea nchini Misri, huku tafsiri ya Juzuu (sehemu) 20 ikiwa tayari imekamilika.

Waziri wa Wakfu Sheikh Mohamed Mukhtar Gomaa alitangaza hitimisho la tarjuma ya Juzuu 20, tovuti ya habari ya El-Balad iliripoti.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya uhusiano wa mambo ya nje ya Bunge la Misri, alisema lengo la tarjuma hiyo ni kukabiliana na mikengeuko na makosa yaliyofanywa na Mayahudi katika tafsiri za awali za Qur'ani Tukufu

Alisema Wizara ya Wakfu iliamua kwamba ilikuwa muhimu kuanza kutayarisha tarjuma ya Qur'ani kwa Kiebrania ili kurekebisha makosa haya.

Kikao cha kamati hiyo kilifanyika kujadili nafasi ya Wizara ya Wakfu katika kukuza mitazamo ya wastani ya kidini katika ngazi ya kimataifa.

Sheikh Gomaa alitaja jitihada za wizara hiyo kukuza heshima kwa wafuasi na vituo vya kidini vya imani nyingine nchini Misri, akibainisha kuwa huduma hiyo imechangia kurejeshwa maeneo ya ibada ya Kiyahudi na Kikristo.

Serikali ya Misri imechukua hatua mbalimbali katika miaka ya hivi karibuni ili kuonyesha taswira ya usawa na uvumilivu wa kidini na kiutamaduni katika nchi hiyo ya Kiislamu ambayo pia ina idadi kubwa ya Wakristo.

 

4101185

Kishikizo: kiebrania ، qurani tukufu ، misri
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha