Akizungumza na IQNA, Abbas Salimi alisema kuwa msafara huo umebeba nafasi ya kipekee kwa wanachama wake kuwafahamisha wafanyaziyara kuhusu sifa na tabia za Qur’ani za Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (AS), kupitia shughuli mbalimbali zikisindikizwa na usomaji wa Qur’ani wa kuvutia na wenye ladha ya kipekee.
“Kwa bahati nzuri, kutokana na ubunifu wa marafiki wenye dhamana, misafara ya Qur’ani sasa inandaliwa wakati wa msimu wa Hija na pia katika matembezi ya Arbaeen, ili kwa uwepo wao katika mazingira haya yenye baraka na mwafaka kwa kuendeleza utamaduni wa Kiislamu na wa Qur’ani, waweze kutekeleza mipango iliyowekwa, ikilenga zaidi usomaji wa Qur’ani na kuandaa makongamano ya kujifahamisha na Qur’ani,” alisema.
Kuhusu Arbaeen na nguvu kubwa inayojitokeza kutokana na umati mkubwa wa wapenzi na wafanyaziyara wa Imam Hussein (AS), Salimi alieleza:
“Kwanza kabisa niseme kuwa harakati na mapambano ya Bwana wa Mashahidi (AS) yalijengwa juu ya Qur’ani na mbinu za kusimama dhidi ya dhulma. Kwa hivyo, kupitia harakati yake ya kishujaa, alidhihirisha upeo wa vitendo wa mafundisho ya Qur’ani—kutokukubali kamwe suluhu na adui kafiri, na wakati huo huo kutokupuuza kwa sekunde moja ibada kwa Neno la Mwenyezi Mungu. Ni kwa sababu hiyo Imam Hussein (AS) alimwomba kaka yake awaombe maadui watoe muda zaidi ili asali na kusoma Qur’ani, kwa kuwa alikuwa na mapenzi makubwa nayo.”
Salimi aliongeza kuwa misingi na malengo haya ya Imam Hussein (AS) yanatoa mfano wa kinadharia na kivitendo kwa wanaharakati wote wa Qur’ani.
“Kile tunachoshuhudia leo kupitia kuzinduliwa kwa misafara ya Qur’ani wakati wa Hija au Arbaeen ni kuwekewa mfumo rasmi na wa kitaasisi unaofungua uwanja wa kuelewa Qur’ani kwa mujibu wa maono ya Mwenyezi Mungu yaliyofundishwa na Maimamu watoharifu (AS), hususan Imam Hussein (AS). Kinachosalia ni kuona ni kwa kiwango gani wanachama wa misafara hii watafaulu kutumia uwezo huu wa kimuundo.”
Alihimiza kuwa wanachama wa msafara hawapaswi kuridhika tu na sauti au lahaja nzuri ya usomaji.
Aliongeza kwamba wawakilishi wa Qur’ani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanapokuwa miongoni mwa umati wa mamilioni ya wapenzi na wafuasi wa harakati ya Abu Abdullah (AS), umati ambao hauishii kwa Waislamu au Mashia pekee, matendo yao lazima yaakisi mafunzo ya Qur’ani.
Maadhimisho ya Arbaeen, ambayo mwaka huu yanaangukia tarehe 14 Agosti, ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani.
Arbaeen huashiria siku ya arobaini baada ya Ashura, siku ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS).
Kila mwaka, mamilioni ya Mashia husafiri hadi Karbala, ambako ndipo makaburi matukufu ya Imam Hussein (AS) yalipo, kushiriki katika ibada na maombolezo.
Wafanyaziyara, hususan kutoka Iraq na Iran, husafiri kwa miguu kwa umbali mrefu hadi katika mji huo mtakatifu.
Iran pia hutuma msafara wa Qur’ani kuelekea Iraq wakati wa matembezi ya Arbaeen. Wanachama wa msafara huu huendesha programu mbalimbali za Qur’ani na kidini, zikiwemo usomaji wa Qur’ani, Adhana, na Tawasheeh, katika barabara ya kati ya Najaf na Karbala na maeneo mengine ya matembezi ya Arbaeen.
Mwaka huu, msafara huo unajulikana kwa jina la Msafara wa Imam Reza (AS).
/3494159/