IQNA

12:24 - May 30, 2020
News ID: 3472817
TEHRAN (IQNA) - Kumezinduliwa Kampeni ya Kimataifa ya kutaka misikiti miwili mitakatifu ya Makka na Madina isimamiwe kimataifa na nchi za Kiislamu.

Kampeni ya Kimataifa ya Kuratibu Usimamizi wa Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka na Madina inayojulikana kama Al Haramain Watch tayari imeshaungwa mkono na wanazuoni wa Kiislamu zaidi ya 100 pamoja na watetezi wa haki za binadamu.

Kampeni hiyo inalenga nchi za Kiarabu na jamii za Waislamu kote duniani kwa lengo la kutaka mjadala kuhusu sera ambazo Saudi Arabia imechukua hivi karibuni kuhusu Hija, Umrah na usimamizi jumla wa misikiti hiyo miwili mitakatifu.

Kwa mujibu wa Al Haramain Watch, ufalme wa Saudi Arbai unakiuka sheria za kwa kuwazuia Waislamu kufika katika misikiti hiyo miwili mitakatifu bila kuwepo ushauriano.

Hatua ya Saudia ya kupiga marufuku ibada ya Umrah bila kushauriana na nchi za Kiislamu au wanazuoni wa Kiislamu duniani inaendelea kukosolewa kote duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, ukoo wa Aal Saud unaotawala Saudi Arabia umetumia vibaya uwenyeji wake wa misikiti hiyo miwili mitakatifu kwa kuwazuia baadhi ya watu au raia wa nchi kadhaa kutekeleza Ibada ya Hija. Mifano ya hivi karibuni na kupigwa marufuku raia wa Qatar kutekeleza Ibada ya Hija na Umrah. Aidha Wairani waliwahi kupiga marufuku kutekeleza Ibada ya Hija na Umrah ambapo marufuku hiyo iliondolewa mwaka 2017. Halikadhalika utawlaa wa Saudia umewawekea raia wa Syria vizingiti katika Ibada ya Hija.

Kati ya wanaoongoza kampeni hiyo ni Sheikh Azmi Abdul Hamid wa Malaysia ambaye anasema ana waraka wa kihisotria ulioandikwa na muasisi wa Saudi Arabia, Mfalme Abdulazizi Bin Saudi ambao unaonyesha kuwa alitaka  nchi zote za Kiislamu duniani ziwe na haki katika usimamizi wa Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka na Madina.

Kampeni ya Al Haramain Watch inafanana na pendekezo la mwaka 2014 la mwanasiasa mmoja Uturuki la kutaka maeneo ya Makka na Madina yasimamiwe kama linavyosimamiwa eneo la Vatican.

3471541

Tags: makka ، madina ، saudi arabia ، Hija
Name:
Email:
* Comment:
* captcha: