Hujjatul-Islam Jafar Fakhr Azar, mtafiti wa historia ya Uislamu wa Kishia, aliandika haya katika makala iliyochapishwa na IQNA kwa mnasaba wa siku za mwisho za mwezi wa Safar na kumbukumbu ya kufariki Mtume Muhammad (SAW). Makala yake ni kama ifuatavyo:
Kufariki kwa Mtume Muhammad (SAW) ni tukio kubwa lililogeuza mwelekeo wa historia ya Kiislamu, likiwa na athari za kihisia, kisiasa, na kijamii. Uchambuzi makini wa tukio hili na tafakuri juu ya tabia za Mtume (SAW) zilizojaa maadili, ubinadamu, na uadilifu unaweza kuwa mwanga wa kuongoza Waislamu wa zama hizi.
Kurudi katika misingi aliyohimiza Mtume (SAW), ikiwemo mshikamano, haki za kijamii, na kuheshimu haki za watu, kunaweza kuisogeza jamii ya Kiislamu mbele katika mshikamo na maendeleo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria vya kuaminika kama vile Seera ya Ibn Hisham na Tabaqat al-Kubra, Mtume Muhammad (SAW) alianza kupoteza nguvu za kukutana na watu katika mwezi wa Safar, mwaka wa 11 Hijria, maradhi yake yalipozidi. Hata hivyo, lililojitokeza zaidi katika siku hizo ni hulka yake tukufu isiyo na kifani.
Hata akiwa mgonjwa, Mtume (SAW) aliwatendea jamaa na marafiki zake kwa upole na unyenyekevu, na hakuwahi kuacha kujali mahitaji ya Umma hata kwa muda mfupi.
Ni jambo la kuzingatiwa kwamba Mtume Mkuu wa Uislamu hakuwahi kuacha jukumu la kuongoza jamii hadi muda wake wa mwisho. Hata katika maradhi yake, alitoa maagizo muhimu kuhusu jeshi la Usama na mambo ya serikali, akionesha kujitolea kwake kwa uadilifu wa kijamii na kulinda haki za watu.
Mtume Muhammad (SAW) daima alisisitiza usawa na kuondoa ubaguzi. Katika nyakati hizo pia alitoa mfano bora wa demokrasia ya kweli kwa kuhimiza heshima kwa makundi yote ya jamii, wakiwemo wanyonge na maskini.
Siku za mwisho za maisha ya Mtume Muhammad (SAW) zilijaa khutba na nasaha zenye hekima. Katika nyakati hizo nyeti, hakujali tu mambo ya serikali, bali pia alikuza mshikamano na huruma katika jamii kwa kusisitiza mshikamo wa Waislamu na kuheshimiana. Wosia wake kuhusu Ahlul-Bayt (AS), Qur’an Tukufu, na kulinda mshikamano wa Ummah unaonyesha undani wa maono yake ya kujenga jamii yenye mshikamano na haki.
Mtume (SAW) alishinda nyoyo kwa ukarimu wake na kwa kujali mahitaji ya kimwili na kiroho ya watu.
Alfajiri ya Safar 28, habari ya kufariki kwa Mtume (SAW) ilipotangazwa, Madina ilitumbukia katika mshtuko. Baadhi ya Masahaba hawakuamini mwanzoni, jambo lililoonyesha undani wa mapenzi ya watu kwa Mtume (SAW) na matokeo ya malezi yake na mapenzi yake yasiyo na kikomo kwa Ummah.
Ukubwa wa msiba huu kwa Ahlul-Bayt (AS) ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba Amirul-Mu’minin Ali (AS) alibeba jukumu la kumfariji Sayyidah Fatimah Zahra (SA) sambamba na kushughulikia mazishi. Tabia ya Imam Ali (AS) katika muda huo, akiendeleza njia ya Mtume (SAW) ya subira, ustahamilivu, na kulinda mshikamano, ilidhihirisha athari kuu ya malezi ya Mtume (SAW) kwa masahaba wake wa karibu.
Tukio la Baraza la Saqifah Bani Sa’idah, lililotokea muda mfupi tu baada ya kufariki kwa Mtume (SAW), lilidhihirisha ukubwa wa changamoto za urithi wa uongozi. Baraza hilo liliitishwa hata kabla ya mwili wa Mtume (SAW) kuzikwa. Tukio hili lilikuwa mwanzo wa mitihani mikubwa iliyotokana na kupotoka kutoka katika misingi ya mshikamano na uadilifu.
Uchambuzi wa kulinganisha baina ya vyanzo vya madhehebu mbali mbali unaonyesha kuwa kuporwa ardhi iliyojulikana kama Fadak na matukio mengine yalitokea muda mfupi baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (SAW), jambo linalohitaji kusomwa upya kihistoria. Haya yote yalidhihirisha jinsi baadhi walivyojiondoa katika nyayo za Mtume Muhammad (SAW) aliyehimiza kuheshimu haki za kila mtu, wakiwemo wanawake na wanyonge.
Mtume (SAW) alitoa mfano wa kivitendo wa jamii yenye uadilifu kwa kusimamia usawa katika mgawanyo wa rasilimali na kuondoa dhulma.
Leo hii, ni lazima tujifunze masomo makubwa kutoka katika tukio hili la kihistoria. Kwanza, ni wajibu kudumisha mshikamano wa Kiislamu kwa mujibu wa wosia wa mwisho wa Mtume (SAW). Alisisitiza mara kwa mara juu ya huruma na kuepuka migawanyiko, na wosia huu unaweza kuwa ufunguo wa kutatua tofauti katika ulimwengu wa Kiislamu leo. Pili, tunapaswa kuiga mfano wake wa uongozi katika nyakati za mitihani. Mtume (SAW) alikabiliana na changamoto kwa hekima, subira, na maadili; mtindo huu ndio bora zaidi kwa jamii za sasa.
Jambo jingine muhimu ni ulazima wa kurudi katika Qur’an Tukufu na watu wa nyumba ya Mtume Muhammad SAW, yaani Ahlul-Bayt AS. Mtume (SAW) alibaini kuwa viwili hivyo, yaani Qur'ani na Ahul Bayt kuwa nguzo mbili kuu. Viwili hivi ni hazina zinazoweza kuokoa Ummah wa Kiislamu kutokana na shimo la migawanyiko. Kadhalika, mfano wa Mtume (SAW) wa kuheshimu haki za watu, wakiwemo wanyonge, wanawake, na maskini, unapaswa kuwa mbele katika sera za kijamii.
Kwa kuunda mazingira yenye uadilifu na huruma, Mtume Muhammad (SAW) alionyesha kuwa mshikamano na uadilifu wa kijamii ndizo funguo za ustawi wa jamii.
3494330