IQNA

Al-Azhar yalaani kitendo cha mwanasiasa Marekani kuteketeza nakala ya Qur'ani

16:57 - August 28, 2025
Habari ID: 3481147
IQNA – Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Misimamo Mikali kimekemea vikali kitendo cha hivi karibuni cha kuchoma nakala ya Qur'ani kilichofanywa na mwanasiasa mmoja wa Marekani.

Kituo hicho kilielezea kitendo hicho kama uchochezi wa makusudi na shambulio dhidi ya imani za kikatifu za Waislamu milioni kwa milioni duniani kote. Taarifa hiyo, iliyoripotiwa na Al-Youm Al-Sabea ya Misri, ilikemea kitendo alichofanya Valentina Gomez, mgombea katika jimbo la 31 la Bunge la Texas, ambaye alijirekodi mwenyewe akichoma nakala ya Qur'ani  Tukufu kwa kutumia kifaa cha moto katika video iliyosambaa kwa haraka. Video hiyo iliandikwa: "Nitamaliza Uislamu Texas, nisaidie Mungu."

Video hiyo ilisambaa kwa haraka mtandaoni na kusababisha hasira kutoka kwa makundi ya utetezi wa Waislamu, viongozi wa kisiasa, na mashirika ya kiraia. "Kitendo hiki ni uchochezi wa makusudi na udhalilishaji wa wazi wa kile Waislamu duniani kote wanachokiheshimu," alisema Al-Azhar. Taasisi hiyo ilionya kwamba vitendo kama hivi vinachochea ugaidi na kuhamasisha makundi ya kitaifa yenye siasa kali kutekeleza uhalifu zaidi wa chuki dhidi ya Waislamu. Katika video yake, Gomez pia alitangaza, "Marekani ni taifa la Wakristo, kwa hiyo wale Waislamu 'magaidi' wanaweza kwenda katika moja ya mataifa 57 ya Kiislamu. Kuna Mungu mmoja tu, na huyo ni Mungu wa Israel."

Kauli hizo zilikutana na kukemewa vikali na kusababisha kufungiwa kwake kwenye mitandao yote mikubwa ya kijamii isipokuwa X. Al-Azhar ilisisitiza kuwa matumizi ya propaganda kali za kisiasa kama hizi zinadhoofisha maadili ya uvumilivu na kuishi kwa amani, huku zikionyesha ongezeko la Chuki Dhidi ya Uislamu au Islamophobia linalochochewa na misimamo ya siasa kali za kulia duniani kote.

Kituo hicho kilitoa wito wa kupitishwa na utekelezaji wa sheria zitakazowajibisha wenye misimamo mikali wanaovunjia heshima Uislamu na Waislamu. Kilisisitiza pia haja ya hatua za kimataifa kukabiliana na kile kilichokitaja kama ongezeko la vitendo vya chuki vinavyohatarisha umoja wa kijamii na usalama wa umma. Hadi sasa, mamlaka za Texas hazijaanza uchunguzi kuhusu kitendo cha Gomez cha kuvunjia heshima nakala ya Qur'ani Tukufu, licha ya kitendo hicho kukemewa vikali. Kwa mujibu wa sheria za Marekani, vitendo kama hivi kwa kawaida vinapewa kinga na kifungu cha Kwanza cha Katiba kinacholinda uhuru wa kutoa maoni, isipokuwa ikiwa vinahusisha vitisho vya moja kwa moja, uchochezi wa vurugu, au uharibifu wa mali.

Pengo hili la kisheria linamaanisha kwamba vitendo vyenye kuchochea uhasama dhidi ya jamii ya kidini—ambavyo vingi vinachukuliwa kama kuchochea chuki na mgawanyiko—vingi hubaki bila adhabu isipokuwa vinapovuka mipaka ya uhalifu.

3494406

captcha