IQNA

Sudan yapuuza malamiko ya wananchi, yafuta sheria ya kuususia biashara na Israel

14:43 - April 07, 2021
Habari ID: 3473790
TEHRAN (IQNA)- Baraza la Mawaziri la Sudan limefuta sheria ya vikwazo na kuususia biashara na utawala wa Kizayuni wa Israel, miezi michache baada ya Khartoum na Tel Aviv kuafikiana juu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili hizo.

Kwa mujibu wa taarifa,  Baraza la Mawaziri la Sudan limesema katika taarifa iliyotolewa jana jioni kuwa, "tumepasisha dikrii ya kutengua sheria ya vikwazo dhidi ya Israel ya mwaka 1958."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, sheria hiyo ya kuondoa vizuizi vya ushirikiano na kufanya miamala na utawala pandikizi wa Israel itawasilishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la Sudan na mawaziri hao kwa ajili ya kupata baraka za mwisho.

Kadhalika Baraza la Mawaziri la Sudan limedai katika taarifa hiyo kuwa, msimamo wa Khartoum kuhusu kuundwa taifa huru la Palestina katika fremu ya uundwaji wa mataifa mawili (Palestina na Israel) ungali thabiti.

Oktoba mwaka jana 2020, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilitangaza kuwa serikali ya mpito ya nchi hiyo imeafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na hivyo kuifanya Sudan kuwa nchi ya tano baada ya Misri (1979), Jordan (1994), UAE na Bahrain (2020) kufikia mapatano na Israel na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni.

Uamuzi huo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel unaendelea kupingwa na kulalamikiwa na makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Sudan, vikiwemo vyama washirika katika muungano tawala nchini humo.

/3962892/

Kishikizo: sudan israel
captcha