IQNA

Saudi Arabia Yazindua Mkutano Mkubwa wa Huduma za Hija kwa Kauli Mbiu ‘Kutoka Makkah Hadi Ulimwenguni’

14:17 - November 10, 2025
Habari ID: 3481495
IQNA – Wizara ya Hija na Umrah ya Saudi Arabia siku ya Jumapili imezindua rasmi Mkutano na Maonesho ya 5 ya Hajj kwa mwaka 1447 Hijria, yanayoendelea kuanzia tarehe 9 hadi 12 Novemba 2025 katika jiji la Jeddah, chini ya kauli mbiu “Kutoka Makkah Hadi Ulimwenguni.”

Maonesho haya yanayofanyika katika ukumbi mkubwa wa Jeddah Superdome yamelenga kuwaleta pamoja wadau wa serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa ili kujadili mustakabali wa utoaji wa huduma za Hija.

Kwa mujibu wa waandaaji, lengo kuu la mkutano huu ni “kuunganisha juhudi za maandalizi ya msimu ujao wa Hija, kuweka mwelekeo wa huduma za baadaye za Hija, na kuinua kiwango cha huduma kwa mahujaji kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya hali ya juu.”

Zaidi ya mataifa 150 na mashirika mbalimbali ya umma na binafsi yanashiriki katika mkutano huu.

Vipengele muhimu vya programu vinajumuisha zaidi ya vikao 80 vya majadiliano na takriban warsha 60 za kitaalamu, huku zaidi ya washiriki 2,400 wakitarajiwa kushiriki katika mafunzo hayo.

4315708

Kishikizo: hija saudi arabia
captcha