
Washiriki kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wamehudhuria mashindano haya ambayo yameandaliwa na Wizara ya Masuala ya Kidini ya Pakistan. Sherehe ya ufunguzi imefanyika katika Ukumbi wa Bunge la Jinnah kwa uwepo wa Waziri wa Masuala ya Kidini wa Pakistan, Sardar Yousaf.
Mashindano haya yamegawanywa katika makundi sita, ambapo mwishoni mwa kila kundi, maqari wawili watachaguliwa kuendelea hatua inayofuata. Nusu fainali zinatarajiwa kufanyika Alhamisi, ambapo washiriki watano watachaguliwa, na fainali zitafanyika siku hiyo hiyo kwa washiriki watatu waliobakia.
Adnan Momenin, qari mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, anawakilisha nchi yake katika mashindano haya. Momenin anatoka mkoa wa Khuzestan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Yeye pia alikuwa mshiriki wa fainali katika Mashindano ya 47 ya Kitaifa ya Qur'ani ya Iran na mshindi wa nafasi ya pili katika mashindano mengine, ikiwemo Tamasha la 27 la Qur'ani na Etrat lililoandaliwa na Wizara ya Afya. Qari maarufu Gholam Reza Shahmiveh ameandamana naye kama mwalimu na mshauri.
Mashindano haya ni sehemu ya juhudi za Pakistan kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni na kiroho miongoni mwa watu wa ulimwengu wa Kiislamu, na kuonyesha nafasi ya Qur'ani Tukufu katika kukuza maadili ya upendo, amani na mshikamano. Kwa kuyapokea mashindano haya, Pakistan inalenga kuonyesha urithi wake wa kiutamaduni, kiroho na kidini, sambamba na kuimarisha uhusiano kati ya nchi wanachama wa OIC.
Aidha, mashindano haya yanakusudia kuwahamasisha vijana kutafakari maana ya Qur'ani na kulinda urithi mtukufu wa usomaji wake kizazi hadi kizazi. Tukio hili litahitimishwa kwa sherehe ya ugawaji zawadi katika Kituo cha Kimataifa cha Mkutano cha Muhammad Ali Jinnah, kwa uwepo wa viongozi wa kidini na wa serikali wa Pakistan, mnamo Novemba 29.
4318937