IQNA

Qari wa Iran Atarajia Ushindani Mkali katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Pakistan

15:07 - November 26, 2025
Habari ID: 3481571
IQNA – Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano ya kwanza ya kimataifa ya Qur’ani nchini Pakistan amesema anatarajia ushindani mkali katika mashindano hayo.

Akizungumza na IQNA akiwa mjini Islamabad, Adnan Momenin alisema kiwango cha washiriki katika mashindano haya, yanayojulikana kama Husn Qara’at (Usomaji Mzuri), ni cha juu kwani kila mmoja tayari ameshiriki katika mashindano kadhaa ya kimataifa. Qari maarufu wa Qur’ani, Gholam Reza Shahmiveh, ameandamana na Momenin katika mashindano haya kama mwongozi. Mashindano haya yalianza mjini Islamabad siku ya Jumatatu na yataendelea hadi Novemba 29.

Momenin, mwenye umri wa miaka 30 na mkazi wa Khorramshahr kusini magharibi mwa Iran, alieleza kuwa mwaka jana alikuwa miongoni mwa washiriki wa fainali za Mashindano ya Kitaifa ya Qur’ani nchini Iran, ingawa hakushinda taji. Hata hivyo, kutokana na ushiriki wake katika fainali hizo, alipata heshima ya kusoma Qur’ani mbele ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwanzoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu. Aidha, Momenin ni mwanachama wa kundi la kimataifa la Misbah-ul-Huda kutoka Abadan. Baada ya kushinda nafasi ya kwanza katika mashindano ya Tawashih, kundi hilo lilialikwa nchini Tanzania mwaka 2017 na mwaka huo huo wakapata heshima ya kusoma mbele ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mwaka 2022, Momenin alihudhuria ibada ya Hija kama sehemu ya msafara wa Qur’ani wa Noor, na katika Ramadhani iliyopita, kundi la Misbah-ul-Huda lilipelekwa nchini China.

Akizungumzia mashindano ya Qur’ani nchini Pakistan, Momenin alisema: “Jina la mashindano haya ni Husn Qara’at, na kwa kuwa yanafanyika kwa mara ya kwanza, inaonekana tutakuwa na ushindani mkali mbele yetu, kwani baadhi ya washiriki tayari wameshinda nafasi katika mashindano kadhaa ya kimataifa.” Wizara ya Masuala ya Kidini ya Pakistan ndiyo inayosimamia mashindano haya ya usomaji wa Qur’ani. Mashindano yalianza Jumatatu, Novemba 24, na yataendelea hadi Ijumaa, Novemba 29. Baada ya sherehe ya kufunga, washindi watatu bora watapewa zawadi na pongezi, na wataalikwa kubaki mjini Islamabad kwa siku tatu zaidi hadi Desemba 3.

Kuhusu ratiba ya usomaji wake, Momenin alisema kuwa baadhi ya washiriki wa makundi ya kwanza na ya pili tayari wamepangiwa kusoma leo au katika siku mbili zijazo, lakini yeye anatarajia kupangiwa siku ya nne ya mashindano haya ya kimataifa.

/3495518

Habari zinazohusiana
captcha