
Naibu Waziri Mkuu Ishaq Dar alikabidhi zawadi kuu — kitita cha rupia milioni tano — kwa Aiman katika hafla ya kufunga mashindano Jumamosi, sambamba na mshindi wa pili Adnan Momenin kutoka Iran na mshindi wa tatu Qari Abdul Rasheed wa Pakistan.
Zaidi ya nchi 37 zilishiriki katika mashindano haya, yakikusanya makari wa Qur’ani chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Kidini ya Pakistan. Mashindano yalifanyika kuanzia Novemba 24 hadi 29 mjini Islamabad, na zawadi zilitolewa katika Ukumbi wa Jinnah Convention Center.
Kwa Aiman, ushindi huu unaongeza safu ya mafanikio ya kimataifa. Mapema mwaka 2025, alishinda taji la Qari wa wanaume katika Mkutano wa 65 wa Kimataifa wa Kusoma na Kuhifadhi Qur’ani Malaysia (MTHQA) mjini Kuala Lumpur.
Mshindi wa pili, Adnan Momeninkhamiseh wa Iran, na mshindi wa tatu Qari Abdul Rasheed wa Pakistan walipokea zawadi za rupia milioni tatu na milioni mbili mtawalia.
Mbali na washindi watatu wa mwanzo, washiriki kutoka Afghanistan, Indonesia na Morocco walishika nafasi ya nne hadi ya sita.
Katika hafla ya kufunga mashindano, Ishaq Dar na Waziri wa Mambo ya Kidini Sardar Muhammad Yousuf waliungana na Qari Syed Sadaqat Ali, jaji mkuu na mratibu wa mashindano, kuwapongeza washindi.
Mashindano haya yanaonekana kama hatua muhimu katika diplomasia ya kidini na kitamaduni ya Pakistan, yakionyesha dhamira ya taifa hilo kuendeleza sanaa ya usomaji wa Qur’ani.
Lengo la mashindano ni kuhamasisha vijana Waislamu duniani kote kuimarisha uhusiano wao na Qur’ani kupitia tajwīd, tarannum na sanaa ya Qira’at.
Mashindano ya mwaka huu yalihusisha makari kutoka nchi wanachama wa OIC, na yakawa mkusanyiko mkubwa zaidi wa kimataifa wa usomaji Qur’ani kuwahi kufanyika nchini Pakistan.
Akihutubia hafla ya kufunga mashindano, Ishaq Dar aliwahimiza waandaaji kuyapanua zaidi, akipendekeza kwamba “mara ijayo makari kutoka kote duniani waalikwe kushiriki.”
Aidha, alitangaza kuwa mashindano hayo yatakuwa tukio la kimataifa la kila mwaka litakalofanyika mjini Islamabad.
3495561