Kwa upande mwingine, Ali Akbar Toupchi alieleza katika mahojiano na IQNA kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani unakaribia. Hivyo, jamii ya wanaoihudumia Qur'ani inapaswa kutafakari juu ya kuandaa mkusanyiko wa mipango madhubuti ili kujaza pengo lililopo na kuhakikisha kuwa shughuli za Qur'ani za Ramadhani zinakuwa zenye tija na manufaa makubwa kwa umma.
Amesema kuwa matukio ya kigaidi ya hivi karibuni yameonesha tena uadui madola ya kibeberu katika uga wa kimataifa dhidi ya misingi ya fikra za kidini. Amebainisha kuwa lau hali hii ingesababishwa na masuala ya kiuchumi, kisiasa au kijamii, isingeelekezwa moja kwa moja kwenye utukufu wa Qur'ani pamoja na maeneo na alama takatifu.
Aidha, aliongeza kuwa mashambulizi dhidi ya vitu vitakatifu, ingawa ni machungu, yamepeleka ujumbe mahsusi kwa wananchi wa Iran, hususan vijana, ambao katika mazingira kama haya wanaweza kufanya maamuzi yasiyo na busara kutokana na propaganda zenye sumu kutoka kwa maadui.
Toupchi alieleza kuwa ujumbe mahsusi ni kwamba adui anapothubutu kuidhalilisha Qurani kwa lengo la kutimiza nia na madhumuni maovu, njama hiyo huishia kuwarudia wao wenyewe, kwa mujibu wa Aya ya 54 ya Surah Al‑Imran.
Akiendelea, alisifu mamilioni ya wananchi waliojitokeza katika maandamano kulaani mashambulizi ya kigaidi na vitendo vya udhalilishaji matukufu ya Kiislamu, akisema: “Wananchi daima wameonyesha kuwa wana upeo, busara na ufahamu wa kutosha katika maeneo nyeti ya Mapinduzi ya Kiislamu, na wana uwezo wa kuyavuruga na kuyazima mipango ya maadui.”
Katika sehemu nyingine ya maelezo yake, mwalimu huyo mkongwe wa Qurani alibainisha kuwa matukio ya kigaidi ya hivi karibuni pamoja na hali ya jumla iliyoenea nchini yamesababisha Mashindano ya 42 ya Kimataifa ya Qurani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuahirishwa hadi wakati mwingine.
Akasema kuwa ni jambo la kawaida kwamba kila mwaka mtazamo wa ulimwengu wa Kiislamu hugeukia Iran ya Kiislamu, kama mwenyeji wa moja ya matukio yenye ushawishi mkubwa katika uwanja wa kimataifa wa Qurani. Kwa hiyo, kutofanyika kwa mashindano hayo kunazua pengo ambalo taasisi husika zinapaswa kulijaza.
Kwa bahati nzuri, mwezi mtukufu wa Ramadhani unakaribia, akaongeza, na hivyo ni jukumu la taasisi na mashirika ya Qura'ni kuchukua hatua mahsusi za kulitukuza Kitabu Kitakatifu katika kipindi hicho kitukufu.
Kwa kufanya hivyo, jeraha lililosababishwa na shambulio la hivi karibuni dhidi ya Qur'ani, ambalo limeacha alama katika nyoyo za Waislamu, litaanza kupona, na pengo lililotokana na kutofanyika kwa mashindano ya kimataifa ya Qurani kwa wakati uliotarajiwa litaweza kufidiwa.
4329122