IQNA

Nchi za dunia zalaani kwa kauli moja hujuma ya Marekani na Israel dhidi ya shule Minab, Iran

11:06 - March 28, 2026
Habari ID: 3482097
IQNA-Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) limelaani shambulio la Marekani na Israel dhidi ya Shule ya Shajareh Tayyebeh katika mji wa Minab, kusini mwa Iran, ambapo angalau wanafunzi na wafanyakazi wa shule 175 waliuawa katika mauaji ya kikatili tarehe 28 Februari.

Katika kikao cha dharura kilichofanyika Geneva siku ya Ijumaa kwa ombi la Iran, China na Cuba, chombo hicho cha kimataifa kimetaka uchunguzi wa  mara moja na kina pamoja  sambamba na kuwajibishwa kwa waliohusika na jinai hiyo.

Katika mkutano huo, maafisa waandamizi wa Iran na wa kimataifa walitoa hotuba, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Türk, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Elimu Farida Shahid, pamoja na mama wa mmoja wa wahanga.

Katika hotuba yake, Türk amelaani shambulio hilo akilielezea kuwa mfano wa kushtua wa athari za vita dhidi ya raia, hasa watoto.

Ametoa pole kwa familia za wahanga, na kusisitiza kuwa mauaji ya wanafunzi hayawezi kuhalalishwa chini ya mazingira yoyote, na akatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka, huru na wenye uwazi ili kubainisha kwa kina kilichotokea na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.

Kwa upande wake, Farida Shahid ameashiria matumizi ya makombora ya Tomahawk yaliyotumika kushambulia shule hiyo, akisema tukio hilo linaweza kuwa mfano wa “uhalifu wa kivita” na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Amesisitiza kuwa shule zina ulinzi maalum kama maeneo ya kiraia, na kwamba mashambulizi dhidi yake yamepigwa marufuku. Pia ametaka maelezo kuhusu mnyororo wa maamuzi uliosababisha shambulio hilo, kufanyika kwa uchunguzi huru, na kubainishwa kwa uwajibikaji wa wahusika. Aidha, ametaja taarifa za awali zinazodokeza uwezekano wa kuhusika kwa vikosi vya Marekani na matumizi ya taarifa potofu, akisisitiza umuhimu wa fidia, msaada kwa waathiriwa, na ujenzi upya wa kituo hicho cha elimu.

Miongoni mwa waliozungumza katika kikao hicho pia alikuwa Mohaddeseh Falahat, mama wa wanafunzi wawili waliouawa shahidi, Mahdieh na Amin Ahmadzadeh. Bi. Falaha aliwakilisha wahanga na manusura wa tukio hilo.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa, alisimulia maumivu ya kuwapoteza watoto wake na kusema janga hilo limeibua majonzi katika familia nyingi zilizokuwa zimewapeleka watoto wao shuleni kwa imani na matumaini. Akiashiria ndoto za watoto hao ambazo hazikutimia na pengo kubwa waliloacha, alitoa wito wa ukweli kuwekwa wazi, wahusika kuwajibishwa, na haki kupatikana. Amesisitiza kuwa madai hayo si kwa ajili ya kulipiza kisasi bali ni kuzuia majanga kama hayo yasijirudie tena siku zijazo.

Katika kikao hicho, karibu nchi 60 pamoja na wawakilishi 19 wa asasi za kiraia pia walizungumza, wakilaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Shule ya Shajareh Tayyebeh.

Wametoa wito wa kuheshimiwa kwa haki za kibinadamu wakati wa mapigano na kusitishwa vita dhidi ya Iran, huku wakisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa haraka, huru na wenye uwazi kuhusu shambulio hilo.

4343012

captcha