
Sayyid Abbas Araghchi ametoa kauli hiyo Ijumaa kwa njia ya video alipohutubu katika kikao cha dharura cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Geneva. Kikao hicho kimeitishwa kujadili shambulio la kigaidi la Marekani na Israel dhidi ya Shule ya Msingi ya Shajare Tayyebeh katika mji wa Minab, kusini mwa Iran, lililosababisha wanafunzi na walimu 175 kuuawa kikatili tarehe 28 Februari.
Araghchi amesema: “Iran leo inajikuta katikati ya dhiki kutokana na vita haramu vilivyolazimishwa na tawala mbili zenye silaha za nyuklia na tabia ya ubabe, yaani Marekani na Israel.
Ameongeza kuwa uchokozi huo “ulio wazi hauna uhalali na ambao umeandamana na ukatili mkubwa” ulianza wakati Tehran na Washington zilikuwa zikishiriki katika mchakato wa kidiplomasia.
Amebainisha kwamba: “Kwa mara ya pili ndani ya miezi tisa, wameisaliti diplomasia kwa kuharibu kabisa meza ya mazungumzo.” Alikuwa akiashiria mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Juni 2025, yaliyotokea wakati kulikuwa na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.
Araghchi ameendelea kusema kwamba: “Miongoni mwa sura za kutisha zaidi za uchokozi huu,” ilikuwa “shambulio lililopangwa kwa makusudi dhidi ya Shule ya Msingi ya Shajare Tayyebeh.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema shambulio hilo dhidi ya shule, ni “uhalifu wa kivita na pia uhalifu dhidi ya ubinadamu,” huku akitoa wito wa “kulaaniwa wazi na bila masharti na kuwajibishwa kwa wale waliohusika.”
Ameongeza kuwa jeshi la Marekani haliwezi kukwepa wajibu kwa kudai tukio hilo ni “ajali” au “makosa ya tathmini.”
Amesema kuwa kulaani shambulio lisilo na huruma dhidi ya mahali pa kiraia, mahali ambapo wasio na hatia zaidi hukusanyika na kutafuta elimu, si tu wajibu wa kisheria chini ya mifumo ya haki za binadamu, bali pia ni wajibu wa kimaadili na wa kibinadamu.
Waziri huyo wa mambo ya nje pia amesema kwamba Shule ya Msingi ya Shajare Tayyebeh siyo mwathirika pekee wa uhalifu wa kikatili wa Marekani na Israel katika kipindi cha siku 27 za vita hivyo haramu dhidi ya Iran. Amesema raia pamoja na miundombinu ya kiraia imelengwa kiholela bila kujali sheria za vita wala misingi ya msingi ya ubinadamu.
Araghchi amesema hadi sasa, zaidi ya shule 600 zimebomolewa au kuharibiwa kote Iran, huku wanafunzi na walimu zaidi ya 1,000 wakiuawa au kujeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo ya Marekani na Israel.
Amesema wavamizi hao pia wameshambulia hospitali, magari ya wagonjwa, wahudumu wa afya, waokoaji wa Hilali Nyekundu, mitambo ya kusafisha mafuta, vyanzo vya maji na maeneo ya makazi.
Araghchi aliwakumbusha waliohudhuria kwamba vita hivi visivyo vya haki vinavyoendeshwa na Marekani na Israel dhidi ya taifa la Iran ni matokeo ya moja kwa moja ya ukimya uliokuwepo mbele ya ukiukwaji wa sheria na vitendo vya kikatili vilivyotokea awali katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Lebanon na maeneo mengine.
Amehitimisha kwa kusema kuwa Iran haijawahi kuanzusha vita na kwamba Wairani ni taifa lenye amani na heshima, linalorithi moja ya ustaarabu tajiri zaidi duniani. Hata hivyo, ameongeza kuwa Wairani wameonyesha azma na uthabiti wa kulinda nchi yao dhidi ya wavamizi wakatili ambao hawana mipaka katika kutekeleza aina mbalimbali za uhalifu—na kwamba ulinzi huo utaendelea kwa muda wote utakaohitajika.
3496901