IQNA

Kongamano Oman Laangazia Nafasi ya Qur’ani katika Maendeleo ya Kimaadili na Kifikra ya Mwanadamu

15:50 - April 21, 2026
Habari ID: 3482157
IQNA – Kongamano la siku mbili linaendelea mjini Muscat, Oman, likilenga kuchunguza nafasi ya Qur’ani Tukufu katika maendeleo ya kifikra na kimaadili ya mwanadamu.

Majadiliano ya kongamano hilo lenye anwani “Qur’ani na Maendeleo ya Mwanadamu”, lililoandaliwa na Wakfu wa Imam Jaber bin Zaid, yalianza Jumatatu chini ya udhamini wa Sayyid Khalid bin Hilal Al Busaidi, waziri wa Diwan ya Mahakama ya Kifalme ya Oman.

Kongamano hilo la siku mbili linakusudia kuangazia mchango wa Qur’ani Tukufu katika kukuza maendeleo ya kifikra na kimaadili ya binadamu, pamoja na kuchunguza uwezekano wa kuimarisha uwepo wake katika kujenga mustakabali wa mwanadamu unaotegemea elimu, maadili na utambulisho.

Likiwa limefanyika katika Chuo Kikuu cha Sultan Qaboos, kongamano hilo linashirikisha wataalamu kadhaa wa elimu za Qur’ani na wanazuoni wa Sharia ya Kiislamu kutoka ndani ya Usultani wa Oman na kutoka mataifa mengine.

Kikao kikuu cha kongamano la “Qur’ani na Maendeleo ya Mwanadamu” kilithibitisha nafasi ya Qur’ani Tukufu kama rejea kuu katika kuunda fikra za mwanadamu na kusimamia uhusiano kati ya elimu na maadili, huku pia kikitoa wito wa kurejeshwa kwa nafasi yake katika kuunganisha mtazamo wa Kiislamu na kuvuka mipasuko ya kifikra.

Majadiliano yalijikita katika umuhimu wa kuwepo kwa uwiano kati ya uelewa wa matukio ya ulimwengu kwa uhalisia na kushikamana na misingi ya maadili, pamoja na kurejesha nafasi ya matumizi ya akili ndani ya mfumo wa Qur’ani unaounganisha elimu na imani. Hali hiyo, kwa mujibu wa washiriki, inaweza kuchangia kujenga mwanadamu aliyesawazika ambaye anashiriki katika ustawi na uhuishaji wa Umma.

Katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, mada ya nafasi kuu ya Qur’ani katika nyanja ya maarifa ya Kiislamu ilijadiliwa kupitia karatasi tano za kitaaluma. Karatasi hizo zilichunguza upeo wa ujenzi wa maarifa na mshikamano kati ya Qur’ani Tukufu, kama rejea ya msingi katika maendeleo ya mwanadamu na ustaarabu—na mbinu nyingine zinazotumika kama vyanzo vya maarifa ya kibinadamu.

Kongamano hilo pia lilijumuisha mihadhara mitatu ya wazi kwa umma iliyojadili mada mbalimbali kwa mtazamo wa Qur’ani. Sambamba na hilo, warsha maalumu ilifanyika kwa anuani “Fiqhi ya Nafsi katika Qur’ani Tukufu: Kujenga Uelewa na Afya ya Kisaikolojia katika Uwanja wa Elimu.” Warsha hiyo iliwasilishwa na Dkt. Abdul Rahman Thakir Al Hashmi.

Warsha hiyo iliwalenga wataalamu wa kijamii na kisaikolojia pamoja na wasimamizi wao kutoka Wizara ya Elimu, ikilenga kutumia mbinu za Qur’ani katika kuimarisha uelewa wa kisaikolojia na kielimu, na kuendeleza utendaji wa kitaaluma unaojengwa juu ya maadili na maarifa yaliyounganishwa.

Kongamano hilo linatarajiwa kutoa mapendekezo kadhaa yatakayochangia kuimarisha uwepo na mchango wa Qur’ani Tukufu katika nyanja mbalimbali za maisha, hususan katika sekta za elimu, ufundishaji na fikra, kwa lengo la kukuza mwanadamu aliyesawazika katika fikra, roho na mienendo.

3497170

Kishikizo: qurani tukufu oman
captcha