IQNA

Mwanazuoni wa Qur’ani wa Iraq: Misimamo ya Qari wa Kuwait yapingana mafundisho ya Mwenyezi Mungu

14:26 - April 26, 2026
Habari ID: 3482164
IQNA – Sheikh Osama Karbalayi, msomaji wa kimataifa wa Qur’ani kutoka Iraq, amesisitiza kuwa misimamo ya qari wa Kuwait, Mishary Rashid Al‑Afasi, katika kuhalalisha uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inapingana na kiini cha mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Mwenye sauti nzuri haondolewi jukumu na uwajibikaji pale anapokuwa sehemu ya kauli au msimamo unaowashambulia wanaodhulumiwa au kunyamazia wanaofanya dhuluma, Karbalayi aliiambia IQNA katika mahojiano yafuatayo:

 IQNA: Kwa kiwango gani misimamo ya hivi karibuni ya Mishary al‑Afasi inaendana na hadithi mashuhuri isemayo: “Huenda wapo wasomaji wa Qur’ani ambao Qur’ani yenyewe inawalaani”?

Karbalayi: Msomaji maarufu wa Qur’ani anapojinasibisha na kauli ya kisiasa inayohalalisha uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, au anaposhambulia harakati ya Kiislamu inayojulikana kwa msimamo wake wa kupinga ukoloni, hilo linatupatia mfano hatari sana wa hadithi hiyo.

Qur’ani si mkusanyiko wa maneno ya kusomwa tu, bali ni mradi wa kimaadili na msimamo wa ustaarabu. Qur’ani inayotaka kuwatetea wanaodhulumiwa na kukataa dhuluma haiwezi kuoana na kauli inayotoa uhalali wa kimaadili kwa wanaofanya mauaji, mzingiro na uchokozi dhidi ya watu wa eneo hili. Kwa hivyo, hatari ya kweli iko katika kuitumia Qur’ani kama chombo ndani ya mazungumzo yanayokwenda kinyume na kiini chake.

IQNA: Ni wajibu gani wa wanaharakati wa Qur’ani, wasomaji na wahafidhi Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu kuhusu mkengeuko huu?

Karbalayi: Wajibu wa kwanza ni kubainisha kwamba Qur’ani haikomei katika usomaji wa sauti tu, na kwamba msomaji wa kweli wa Qur’ani ni yule ambaye misimamo yake kuhusu masuala yanayolikabili Ummah inaundwa na aya za Qur’ani.

Jamii ya Qur’ani haiwezi kunyamaza wakati umaarufu wa Qur’ani wa mtu unapotumiwa kama jukwaa la kuhalalisha uchokozi au kushambulia nguvu ambazo zimelipa gharama kubwa katika kutetea uhuru wa Ummah. Aidha, ni lazima kuwasilisha mifano angavu ya Kiislamu inayochanganya uzuri wa usomaji na ufahamu wa kiitikadi na kimaadili, ili msikilizaji asivutiwe na sauti pekee bila kuelewa maana.

Kulinda mafundisho ya Qur’ani leo ni jukumu kubwa, kwa sababu mkengeuko kutoka katika haki, hasa ukitoka kwa mtu mashuhuri, unaweza kuwa na athari mbaya zaidi kuliko mkengeuko wa kisiasa wa watu wa kawaida.

IQNA: Kwa nini mtu kama al‑Afasi, anayejulikana kwa sauti yake nzuri, achukue misimamo kama hii?

Karbalayi: Kuwa na sauti nzuri hakumaanishi kuwa na upeo wa kina au msimamo ulio sawia. Imani na misingi ya kisiasa huathiri sana maamuzi na mitazamo ya watu. Mtu anapoathiriwa na mazingira ya kiitikadi yanayoona mhimili wa mapambano kuwa adui mkubwa kuliko wakaliaji, ni jambo la kawaida kuvutiwa na kauli zinazoishambulia Iran na kuafikiana na tawala zinazokwepa makabiliano ya moja kwa moja na mradi wa Marekani na Kizayuni.

Hivyo tunaona misimamo yao ikiwa mikali dhidi ya mhimili wa mapambano, huku ikionyesha udhaifu mkubwa au ukimya wa wazi kuhusu mauaji, mzingiro na uharibifu uliotokea na unaoendelea huko Gaza, Yemen na Iraq.

IQNA: Tunapaswa kufanya nini ili kunufaika na elimu safi ya Qur’ani na kuepuka mkengeuko?

Karbalayi: Kinachohitajika ni kujenga upya uhusiano wetu na Qur’ani kwa msingi wa tafakkuri, uelewa na kujitoa, si kwa sauti nzuri pekee. Ummah unamhitaji msomaji anayeishi Qur’ani kabla ya kuisoma, na anayefanya aya zake kuwa kipimo cha matendo, si yule mwenye sauti ya kuvutia tu.

Ni lazima tuandae vizazi vinavyoelewa kwamba Qur’ani inaunganisha usomaji na uadilifu, kuhifadhi na ufahamu, na uzuri wa sauti na ukamilifu wa maadili. Kwa sababu mkengeuko hatari zaidi ni kuinua sauti ya Qur’ani ilhali kiini chake hakionekani katika matendo ya mhusika.

3497231

captcha