
Akizungumza katika mahojiano na IQNA, Muhammad Hassan Ali al‑Kabari alipendekeza kwamba ususiaji wa kitaaluma dhidi ya al‑Afasi ushughulikiwe kwa uzito na kwamba kumwalika katika mikutano rasmi kusimamishwe.
Al‑Kabari alisema kuwa msimamo wa al‑Afasi na wanaomuunga mkono, ambao Shetani amewashinda, ni msimamo wa kudhalilisha na wa ajabu; kwa sababu wamekaa kimya mbele ya damu ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, watu wa Iran, Lebanon na Palestina, na wanashirikiana katika dhuluma na uchokozi dhidi yetu sisi Waislamu. Akaongeza kuwa haishangazi kuwa wanajikuta katika safu moja na watenda jinai makatili, Benjamin Netanyahu na Donald Trump.
Aliongeza kuwa uchochezi wa mtu mwenye ushawishi kama al‑Afasi kutadhuru umoja wa Kiislamu, kutasababisha kudhoofika kwa imani kwa taasisi za kidini, na pia kuchafua taswira ya Uislamu duniani na kuchochea hali ya chuki dhidi ya Uislamu.
Alipoulizwa kuhusu wajibu wa wanaharakati wa Qur’ani, wasomaji na wahifadhi wa Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu mbele ya msimamo huu uliopotoka, al‑Kabari alisema makundi hayo yanapaswa kuchukua msimamo thabiti wenye kulenga marekebisho, na kutoa tamko la kuunga mkono heshima na utukufu wa Qur’ani dhidi ya mienendo ya kudhalilisha Neno la Wahyi.
Alisema pia kuwa hatua kadhaa zinapaswa kuchukuliwa, kama vile kuwasiliana moja kwa moja na al‑Afasi ili kumweleza makosa yake kwa mtazamo wa kidini na kijamii, na kumwita atubu na aombe radhi hadharani, huku zikifafanuliwa misingi ya maadili na dini ambayo wabebaji na watu wa Qur’ani wanapaswa kuizingatia kwa ajili ya kuelimisha jamii. Pia akataja kususia kitaaluma kwa kusimamisha kumwalika al‑Afasi katika mikutano rasmi na vikao vya Qur’ani hadi pale atakaporekebisha mwenendo wake, na kuepuka kumpa uhalali katika kupotoka kwake.
Qari huyo wa Yemen aliendelea kusema kuwa kuimarisha vielelezo bora kwa kuzingatia kuwatambulisha vijana mifano ya kweli ya wasomaji wanaochanganya usomaji mzuri wa Qur’ani na maadili mema ni hatua nyingine muhimu inayopaswa kuchukuliwa.
Akizungumzia haja ya kuondoa qira’a za msomaji huyo wa Kuwait katika mitandao ya redio na televisheni pamoja na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, al‑Kabari alisema: “Ninaunga mkono kuondolewa kwa qira’a za al‑Afasi ili apate kutambua uzito wa jambo hili. Wajibu wa wasomaji wa Qur’ani, wahifadhi wake na wanaharakati wa vyombo vya habari pia ni kuonya kuhusu kupotoka kwa misimamo ya al‑Afasi.”
Alipoulizwa kuhusu mwitikio wa maoni ya umma na wanaharakati wa Qur’ani nchini Yemen kuhusu tukio hili, alisema kuwa wasomaji wa Qur’ani na wanaharakati wa Yemen wameweka wazi misimamo yao na wametangaza kujitenga na al‑Afasi; kama vile watu huru katika ulimwengu wa Kiislamu walivyotoa misimamo iliyo wazi na ya heshima katika suala hili. Akakumbusha kauli ya Mwenyezi Mungu katika Aya ya 18 ya Surah Al‑Hajj: “Na ambaye Mwenyezi Mungu anamfedhehesha, basi hana wa kumpa heshima.”