Kwa mujibu wa IQNA, Hujjatul Islam Ahmad Sharafkhani Mkuu wa Idara ya Utamaduni na Masuala ya Kijamii katika Shirika la Awaqf la Iran ameyasema hayo pembizoni mwa Awamu ya 38 ya Mashindano ya Kitaifa ya Qur'ani Iran yanayofanyika katika mji wa Kermanshah magharibi mwa nchi.
Amesema kushiriki idadi kubwa ya watu katika warsha maalumu za kuhifadhi Qur'ani ni ishara ya kuwepo azma imara ya kustawisha harakati za Qur'ani katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Iran ilianza kutekeleza 'Mpango wa Kitaifa wa Kuhifadhi Qur'ani' miaka minne iliyopita baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutoa wito wa kuwepo watu milioni 10 waliohifadhi Qur'ani nchini.
Mpango huo wa kuhifadhi Qur'ani unatekelezwa kwa ushirikiano wa taasisi kadhaa Iran ikiwa ni pamoja na Wizara ya Elimu, Shirika la Utangazaji la Iran IRIB na Wizara ya Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu.
Kwingineko katika matamshi yake Hujjatul Islam Sharafkhani amesema mashindano ya kitaifa ya Iran ni tukio kubwa zaidi la Qur'ani kitaifa na ni dhihirisho la upana wa harakati za Qur'ani nchini.
Awamu ya 38 ya Mashindano ya Kitaifa ya Qur’ani Iran yameanza Jumamosi ambapo kuna washiriki zaidi ya 630 wakiwemo maqarii na waliohifadhi Qur’ani kutoka maeneo yote ya Iran watakaoshiriki katika mashindano hayo ya wiki moja.