IQNA

Iran yalaani hujuma za kigaidi Saudi Arabia

16:51 - July 05, 2016
Habari ID: 3470434
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani hujuma za kigaidi zilizojiri Jumatatu Saudi Arabia likiwemo ikiwemo karibu na Msikiti wa Mtume SAW katika mji mtakatifu wa Madina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qasemi ametuma salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa familia za wahanga wa mashambulizi hayo na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani ugaidi wa aina zote na popote pale unapotokea duniani na unazitaka nchi zote kupambana kwa nguvu zote na vyanzo, sababu na wanaofanya mashambulizi ya kigaidi.

Qasemi amesema kuwa ugaidi hususan katika Mashariki ya Kati umeonesha kuwa, ovu hilo halitambui mipaka wala utaifa na hakuna njia nyingine ya kukabiliana nalo isipokuwa mshikamano na umoja wa kimataifa.

Naye Waziri wa Mambo ya Iran Mohammad Javad Zarif katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa twitter amesema magaidi hawana mistari myekundu tena na kwamba Waislamu wote wa madhehebu ya Shia na Sunni wanalengwa na hivyo kunapaswa kuwa na umoja kukabiliana na ugaidi.

Magaidi wawili waliokuwa na mabomu jana jioni walijilipua karibu na Masjidu Nabawi mjini Madina na katika msikiti mwingine wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Qarif huko mashariki mwa Saudia. Mashambulizi hayo yaliyotekelezwa na magaidi wakufurishaji wa Kiwahhabi yamesababisha vifo vya watu wasiopungua sita na kujeruhi wengine kadhaa.

3513065

captcha