
Kwa mujibu wa Chama cha Madaktari wa Sudan, shambulio hilo lilitekelezwa na kundi la waasi linalojul;ikana kama Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF), na limezua ghadhabu kubwa miongoni mwa wananchi pamoja na kuibua upya wasiwasi kuhusu kulengwa kwa makusudi kwa raia wasiokuwa na hatia katika mzozo unaoendelea nchini humo.
Shambulio hilo lililenga kituo cha elimu ya kiraia kilichopo katika mji wa Rahad, ambacho kilikuwa kinatumika pekee kwa ajili ya elimu ya kidini na uhifadhi wa Qur’ani Tukufu. Mashambulizi hayo yalifanywa kwa kutumia ndege zisizo na rubani licha ya kutokuwepo kwa matumizi yoyote ya kijeshi katika eneo hilo.
Tukio hili limeibua hisia kali, likionesha kwa uwazi hali ya vita isiyochagua kati ya raia na wapiganaji, tangu kuzuka kwa mapigano nchini Sudan mnamo Aprili 2023. Maeneo ya kiraia, ikiwemo shule, misikiti, vituo vya kidini na makazi ya watu, yameendelea kulengwa kadiri mapigano kati ya pande hasimu yanavyozidi kushika kasi.
Ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa na mashirika ya kibinadamu zimethibitisha ongezeko kubwa la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika eneo la Kordofan katika miezi ya hivi karibuni, huku watoto wakionekana kuwa miongoni mwa waathirika wakuu. Hali hii imewalazimu mamia ya maelfu ya raia kuyahama makazi yao kutokana na kuzorota kwa usalama.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), makumi ya maelfu ya watu wamekosa makazi katika wiki chache zilizopita pekee, huku ghasia zikienea katika maeneo ya kati na magharibi mwa Sudan.
Vita vinavyoendelea vimezidisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu uliokuwapo tayari. Raia wanakabiliwa na njaa iliyoenea, kusambaratika kwa miundombinu ya msingi, na ukosefu mkubwa wa usalama. Kulengwa kwa taasisi za elimu na dini kumeongeza zaidi hofu kuhusu usalama wa raia, hususan watoto na wanafunzi wa elimu ya Kiislamu.
Habari inayohusiana:
Licha ya wito wa mara kwa mara kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu kulindwa kwa raia, mashambulizi dhidi ya malengo yasiyo ya kijeshi yanaendelea bila kusita. Matukio ambayo watoto wanapoteza maisha yao yanabaki kuwa ukumbusho mzito wa wajibu wa kisheria na kimaadili wa pande zote chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.
Waangalizi wa masuala ya kikanda wanaonya kuwa bila kusitishwa kwa mapigano kwa njia ya kudumu na kuanzishwa kwa mchakato wa kisiasa wa kweli, hatari ya kutokea kwa majanga kama haya nchini Sudan itaendelea kuwa kubwa.
Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa inawaunga mkono waasi hao wa RSF ambao walianzisha vita vya kunyakua madaraka Aprili 2023. Hadi sasa vita hivyo vimepelekea makumi ya maelfu ya Wasudani wasio na hatia kuuawa na wengine zaidi ya milioni 12 kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.
3496386