IQNA

Mfungwa wa kisiasa Bahrain afariki baada ya kunyimwa matibabu

23:38 - April 08, 2021
Habari ID: 3473794
TEHRAN(IQNA)- Mfungwa wa kisiasa nchini Bahrain amefariki baada ya wakuu wa gereza alimokuwa kukataa kumpa huduma za dharura za kiafya huki hali ikiripotiwa kuwa mbaya katika gereza za nchi hiyo kutokana na janga la COVID-19.

Chama kikuu cha upinzani nchini Bahrain, Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al-Wefaq, imetoa taarifa na kusema Abbas Malallah alifariki katika gereza la kuogofya la Jau ambapo viongozi wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu na wafungwa kiitikadi wanashikiliwa. Taarifa hiyo imesema Malallah amefariki kutokana na kunyimwa huduma za kitiba na pia hali hatari na iliyo dhidi ya ubinadamu katika gereza hilo.

Malallah amezikwa katika kijiji chake cha Nuwaidrat yapata kilomita 10 kutoka mji mkuu wa Bahrain, Manama. Ameacha mjane na watoto watatu.

Kufuatia kifo cha Malallah, wapinzani wa ufalme wa kiimla wa Bahrain wameandamana maeneo mbali mbali ya nchi hiyo hasa katika vijiji vya Hamala, Abu Saiba, Shakhura, Bani Jamra, Northern Sehla, Karrana, Dumistan, Karzakan, Karbabad, al-Dair na pia katika miji ya Samaheej na A’ali .

Waandamanaji walionekana wakiwa wamebebe picha za jamaa zao wanaoshikiliwa katika magereza ya ufalme na wametaka wafungwa hao wote wa kisiasa waachiliwe huru kutokana na kuenea COVID-19 magerezani.

Malallah alikamatwa Mei 17 mwaka 2011 kwa tuhuma za kushiriki katika maandamano dhidi ya ufalme wa ukoo wa Aal Khalifa na alihukumiwa kifungo cha miaka 15.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiisamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

3474396

Kishikizo: bahrain maandamano
captcha