IQNA

Salamu za rambirambi za rais wa Iran kufuatia kuaga dunia Ayatullah Saeed Al Hakim

19:24 - September 04, 2021
Habari ID: 3474257
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim wa Iraq.

Katika ujumbe wake, Rais Sayyid Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemuomboleza mwanazuoni na faqihi wa ngazi za juu Ayatullahil Udhma Sayyid Saeed Hakim na kusema: "Marjaa huyu wa kidini alikuwa mmoja kati ya nguzo za kifiqhi na marjaiya nchini Iraq alikonawiri na alitumia umri wake uliojaa heshima katika njia ya kueneza Uislamu na fikra za Ahul Bayt (AS)."

Aidha rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapambano ya mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kutetea haki za taifa la Iraq yalipelekea afungwe miaka mingi gerezani wakati  wa utawala wa Kibaath wa Saddam na hivyo katika historia ya mapambano ya watu wa Iraq anatazamwa kama mfano wenye kutegemewa wa namna ambavyo Maulamaa wa Kiislamu daima wako pamoja na wananchi.

Aidha Rais Raisi amesema Ayatullah Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim pamoja na watu wengine wa ukoo mkubwa wa Al Hakim alikuwa na nafasi kubwa katika kuunga mkono wananchi wa Iraq na kuwawezesha kupata uhuru na kujitegemea sambamba na kuhakikisha wananchi wenyewe wanajiamulia hatima yao wakiwa na umoja katika Iraq mpya.

Ayatullah Sayyid Mohammad Saeed Tabatabai Hakim Marjaa Taqlid maarufu katika mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq aliaga dunia Ijumaa kutokana na mshtuko wa moyo.

130987

captcha