IQNA

Matembezi ya Arbaeen yaanza rasmi kusini mwa Iraq, kutoka Ras al-Bisheh hadi Karbala

17:18 - July 14, 2025
Habari ID: 3480940
IQNA – Hijra ya Arbaeen ya mwaka 1447 Hijria imeanza rasmi, huku maelfu ya mahujaji wakiianza safari yao kwa miguu kutoka eneo la Ras al-Bisheh, lililoko kusini kabisa mwa Iraq katika mkoa wa Al-Faw, wakielekea mji mtakatifu wa Karbala.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iraq, wafanyaziara wameanza matembezi yao marefu katika joto kali la kiangazi, wakielekea kwenye haram ya Imamu Hussein (Alayhis Salaam). Ras al-Bisheh inajulikana kuwa ndio mwanzo wa mbali kabisa wa safari ya Arbaeen ndani ya mipaka ya Iraq, safari inayokadiriwa kuwa na umbali wa zaidi ya kilomita 600 hadi Karbala.

Licha ya joto kali kufikia zaidi ya nyuzi joto 50 za Selsiasi, vikundi vikubwa vya wafanyaziara tayari wameanza safari yao, wakifungua mlango wa wiki kadhaa za maadhimisho ya Arbaeen, siku ya 40 baada ya Ashura, ambayo mwaka huu itaangukia tarehe 14 Agosti.

Tukio hili la kila mwaka ni ukumbusho wa kufa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (Rehma na Amani Zimshukie na Watu wa Nyumba Yake), aliyeuawa katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia. Arbaeen ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani, ikiwasilisha mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kutoka Iraq na nchi jirani.

Kwenye njia ya kwenda Karbala, mawkib, vituo vya kujitolea vinavyoandaliwa na jamii na vikundi vya kidini, vimewekwa ili kuwahudumia wafanyaziara kwa kuwapa chakula, maji, huduma za afya, na mahali pa kupumzika.

Mwaka jana, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa haram tukufu ya Imam Hussein (AS), zaidi ya wafanyaziara milioni 21 walishiriki katika maandamano ya Arbaeen.

Safari hii ya kuelekea Karbala haichukuliwi tu kama matembezi ya kimwili, bali pia ni ibada ya kiroho na ishara ya mshikamano na maadili ya haki, kujitolea, na sadaka ambayo Imamu Hussein (AS) alisimamia.

4294252

captcha