IQNA

Ashura

Leo ni Siku ya Ashura, Waislamu waomboleza kuuawa shahidi Imam Hussein AS

13:26 - August 08, 2022
Habari ID: 3475595
TEHRAN (IQNA)- Leo ni Jumatatu tarehe 10 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria Qamaria inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 2022. Hii ni Siku ya Ashura ambapo Waislamu na wapenda haki kote duniani hukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake katika jangwa la Karbala.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku kama ya leo.

Kwa mnasaba wa siku hii Mamilioni ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejiunga na wenzao kote duniani kwenye vikao vya maombolezo kukumbuka dhulma waliotendewa mashahidi wa Karbala katika Siku ya Ashura.

Waombolezaji kote Iran wakiwa wamevalia nguo nyeusi kama ishara ya maombolezo walikuwa wakibubujikwa na machozi kwa majonzi na huzuni kwa dhulma iliyofanywa na madhalimu dhidi ya kizazi bora cha wanadamu.

Wairani wanaoshiriki katika maombolezo ya Siku ya Ashura husikiliza hotuba na mashairi kuhusiaiana na masaibu yaliyomkumba Imam Hussein AS huko Karbala. Katika siku hii idadi wafadhili hujitolea kuwalisha mamilioni ya waumini ambapo chakula hicho ni maarufu kama Nazri.

Huko Karbala, Iraq idadi kubwa ya waumini kutoka maeneo yote ya dunia pia wamejitokeza kukukumbuka masaibu ya Imam Hussein AS katika Siku ya Ashura. Katika nchi za Kiafrika kama vile Nigeria, Tanzania, Kenya, Uganda na Afrika Kusini pia kumefanyika mijumuiko ya Siku ya Ashura.

Mafunzo ya harakati ya Imam Hussein AS yamesambaa na kutanda katika historia na jiografia ya viumbe, wanadamu na ulimwengu mzima na hayawezi katu kuishia kwenye mipaka maalumu.

Kishikizo: ashura ، imam hussein as ، karbala
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha