IQNA

Surat al-Fajr yadhihirisha Falsafa ya Ashura, asema profesa wa masomo ya Kiislamu

17:43 - July 09, 2025
Habari ID: 3480918
IQNA – Mwanazuoni mmoja kutoka Iran ameelezea kuwa Surat al-Fajr katika Qur'an Tukufu ni sura iliyo na uhusiano wa karibu sana na urithi wa Imam Hussein (AS), akiitaja kuwa ni tafakuri ya kina kuhusu falsafa ya mapinduzi ya Karbala.

Akizungumza katika kikao cha mwisho cha semina ya mtandaoni yenye kichwa “Uongozi wa Ki-Qur’ani na Mapinduzi ya Imam Hussein (A.S)” siku ya Jumanne, Hujjatul Islam Najaf Lakzaei, Rais wa Taasisi ya Sayansi za Kiislamu na Utamaduni na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Baqir al-Ulum, alisema:
“Katika maneno ya Ahlul Bayt (AS), hasa Imam Sadiq (AS), Surat al-Fajr inajulikana kama sura ya Imam Hussein (AS).”

Alifafanua kuwa sura hii ya Qur’ani inahusishwa na kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) pamoja na maswahaba wake waliouawa katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria.

“Aya za mwanzo, ‘Na kwa Alfajiri, na kwa masiku kumi’, zinaashiria kuibuka kwa nuru juu ya giza. Mfasiri wengi wameeleza kwamba hii inaonesha namna kujitolea kwa Imam Hussein (A.S) kulivyomaliza giza la kiroho lililokuwa limetanda juu ya Uislamu,” alisema Lakzaei.

Kwa mujibu wake, mapinduzi ya Imam Hussein (AS) yaliokoa Uislamu usiangamie chini ya utawala wa Yazid kutoka ukoo wa Umawiyah.
“Kama mapinduzi haya yasingetokea,” aliongeza, “kama alivyoonya Imam Hussein (AS) mwenyewe, basi Uislamu ungebatilika kabisa chini ya utawala wa Yazid.”

Lakzaei alieleza kuwa kuna tabaka tatu za tafsiri zinazounganisha sura hii ya Qur’an na Imam Hussein (AS) Kipengele cha pili, alisema, kinaonekana katika aya zinazozungumzia madhalimu wa kale kama ‘Ad, Thamud na Firauni waliotajwa ndani ya sura hii.
“Walikuwa na nguvu kubwa na mamlaka, lakini walijaribu kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu na walipinga Mitume Wake,” alisema. Aliwafananisha na Yazid, akisema kuwa Yazid ni sehemu ya mlolongo wa madhalimu wa kihistoria, ilhali Imam Hussein (AS) yuko upande wa Mitume na waokozi wa historia.

Kipengele cha tatu na chenye umuhimu mkubwa zaidi, alisema Lakzaei, kinapatikana katika aya za mwisho za sura:

“Ewe nafsi iliyo na utulivu, rudi kwa Mola wako ukiwa radhi na umeridhiwa. Basi ingia miongoni mwa waja Wangu. Na uingie Peponi Mwangu.” (Aya ya 27-30)

Alisema kuwa kwa mujibu wa hadithi, aya hizi zinamhusu Imam Hussein (AS), ambaye alifikia hali ya juu kabisa ya nafs al-mutma’inna (nafsi iliyo na utulivu), na akapata daraja la kiroho la rāḍiya mardiyya—yaani kuridhika na amri ya Mwenyezi Mungu na kuridhiwa na Mwenyezi Mungu.

3493760

captcha