Tukio la Rakdha Tuwairaj hufanyika kila mwaka Karbala katika Siku ya Ashura, ambapo wafanyaziara hukimbia kwa umbali wa kilomita 2–3 kuelekea kwenye kaburi tukufu la Imam Hussein (AS) kukumbuka mbio walizokimbia watoto wa shangazi wa Abul Fadhlil Abbas (AS) wakitoka kijiji cha Tuwairaj (sasa kinajulikana kama Al-Hindiya) hadi Karbala baada ya tukio la mauaji ya siku ya Ashura.
Katika maandamano ya mwaka huu, maelfu kwa maelfu ya waombolezaji waliingia kwa kukimbia hadi katika makaburi matukufu ya Imamu Hussein (AS) na Abul Fadhlil Abbas (AS) huku wakitoa kauli ya hamasa: "Labbayka Ya Hussein!"
Mojawapo ya mambo yaliyovutia sana mwaka huu ilikuwa ni uwepo wa picha nyingi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Sayyid Ali Khamenei sambamba na Ayatollah Mkuu Sistani, kiongozi wa kidini wa Mashia nchini Iraq, mikononi mwa waombolezaji.
Washiriki wa maombolezo haya hukusanyika katika eneo la Qantara al-Salam lililo karibu na kijiji cha Tuwairaj na kuanza safari yao ya kiroho hadi kwenye Haram ya Imamu Hussein (AS), wakiimba kwa sauti ya shauku "Labbayka Ya Hussein", wakijibu wito wa kihistoria wa Imamu Hussein (AS) siku ya Ashura: "Hal min Nasirin Yansurna?" (Je, yupo mwenye kutunusuru?).
Kwa mujibu wa wanahistoria, tamaduni hizi zilianza kati ya mwaka 1855 au 1872 Miladia, zikianzishwa na mtu aitwaye Mirza Saleh Qazvini ambaye alianza kufanya majlisi za maombolezo katika nyumba yake eneo la Hendiyeh au Tuwairaj katika siku kumi za kwanza za Muharram. Katika siku ya Ashura, waombolezaji walitoka nyumbani kwake na kuelekea makaburi matukufu.
Waislamu wa Kishia na wengine duniani huadhimisha kila mwaka shahada ya Imam Hussein (AS) katika mwezi wa Muharram wa kalenda ya Hijria ya mwezi, ambao mwaka huu ulianza tarehe 27 Juni.
Imam Hussein (AS), Imamu wa tatu wa Kishia, pamoja na familia na maswahaba wake waliuawa shahidi katika ardhi ya Karbala mnamo tarehe 10 ya Muharram mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia, mikononi mwa jeshi la Yazid bin Mu'awiya.
3493730