IQNA

Mapinduzi ya Imam Hussein (AS) yalikuwa ni kusimama dhidi ya unafiki na dhulma

16:12 - July 02, 2025
Habari ID: 3480882
IQNA – Mwanazuoni mashuhuri kutoka Iran amesisitiza umuhimu mkubwa wa mapinduzi ya Imam Hussein (AS) katika kufufua uhai wa Uislamu wa kweli na kufichua unafiki uliokuwa umejificha ndani ya umma wa Kiislamu.

Akizungumza katika mkutano wa wasomi uliofanyika Qom siku ya Jumanne, Hujjatul Islam Najaf Lakzaei, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Baqir al-Olum, alielezea mapinduzi ya Imam Hussein (AS) kuwa ni kielelezo cha uongozi wa Ki-Qur’ani na mfano wa kusimama imara dhidi ya dhulma na uonevu. Tukio hilo lilikuwa sehemu ya tatu katika mfululizo wa mijadala kuhusu uongozi wa Qur’ani na urithi wa Imam Hussein (AS).

“Imam Hussein (AS), kupitia mapambano na hatimaye kuuawa shahidi, hakutetea tu Uislamu, bali aliwaonesha wanadamu wote kuwa njia ya Yazid bin Muawiya na wafuasi wake haikuwa na uhusiano wowote na ujumbe wa kweli wa Uislamu,” alisema mwanazuoni huyo.

Hujjatul Islam Lakzaei, ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Sayansi za Kiislamu na Utamaduni ya Qom, alieleza kuwa mapinduzi ya Imam Hussein (AS) hayakuchochewa na matamanio ya binafsi. “Tangu mwanzo wa harakati yake, Imam Hussein (AS) alitangaza wazi kuwa hakusimama kwa ajili ya ubinafsi,” alisema. “Lengo lake lilikuwa ni kuendeleza mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam Ali (AS), kwa nia ya kuleta islah (marekebisho) katika jamii ya Kiislamu.”

Alionya kuwa hatari kubwa kwa jamii ya Kiislamu haiji kutoka kwa maadui wa nje, bali inatoka ndani. “Tishio kubwa zaidi kwa umma wa Kiislamu ni unafiki na wanafiki.”

Kwa mujibu wa Hujjatul Islam Lakzaei, Qur’ani imeeleza mara nyingi kuhusu hatari hii ya ndani katika sura kama al-Baqara, al-Tawba, na al-Munafiqun. “Qur’ani imeweka wazi kuwa tishio linalotokana na wanafiki ni kubwa zaidi kuliko la makafiri wa wazi,” alifafanua. “Kufuru ya wazi inaeleweka na Waislamu, lakini unafiki, ambao umejificha chini ya kivuli cha dini, unasaliti Uislamu kutoka ndani.”

Akinukuu aya kutoka Surah al-Mumtahina, Hujjatul Islam Lakzaei alieleza kuwa hata makafiri wamegawanywa na Qur’ani. “Qur’ani inatofautisha kati ya wale wenye uhasama na wasiokuwa na uhasama. Wale wasiokuwa maadui wanaweza kutendewa kwa uadilifu. Lakini wanafiki wanaojifanya Waislamu na kuapa kwa jina la Allah, lakini hawana imani ya kweli, ni hatari zaidi.”

“Huu ndio mkondo hatari ambao Imam Hussein (AS) alikabiliana nao kwa ujasiri mkubwa,” alisema Lakzaei. “Alifichua utawala wa unafiki na kuonesha wazi kuwa utawala wa Yazid ulikuwa ni dhalimu, fisadi, na haukuwa na uhusiano wowote na uongozi wa Qur’ani.”

Hujjatul Islam Lakzaei alieleza kuwa uongozi wa kweli wa Ki-Qur’ani, kama ulivyoonekana kwa manabii kama Nabii Yusuf (AS), Talut, Nabii Suleiman (AS), na Dhu al-Qarnayn, unajengwa juu ya haki na kukataa batili. “Mtume Muhammad (SAW) na Imam Ali (AS) waliendeleza njia hiyo hiyo, lakini wanafiki wamekuwa kikwazo daima  na bado wanaendelea kuwa hivyo.”

Alisema kuwa kiwango cha juu cha unafiki kilionekana pale baadhi ya makundi yaliposimama wazi dhidi ya Imam asiye na kosa. “Wanafiki hawakuanza na Imam Hussein (AS) peke yake. Walimpinga pia Mtume (SAW), Imam Ali (AS), na Imam Hassan (AS). Hatimaye, walikusanyika kumkabili Imam wa haki huko Karbala.”

Akizungumzia hali ya sasa katika ulimwengu wa Kiislamu, Hujjatul Islam Lakzaei alisema, “Leo hii, ulimwengu wa Kiislamu bado unakumbwa na unafiki. Wapo wale wanaojionesha kuwa Waislamu, lakini wanashirikiana kwa siri na maadui wa Uislamu. Wanavuruga umoja wa ummah wa Kiislamu. Wengine hata wanadai kuwa wanasimama na Palestina, lakini wanakutana faraghani na Wazayuni.”

3493684

 

Habari zinazohusiana
Kishikizo: imam hussein as ashura
captcha