IQNA

Jinai za utawala haramu wa Israel

Januari 19; Siku ya Ghaza ni Kielelezo cha Mapambano ya Kiislamu

20:49 - January 19, 2023
Habari ID: 3476430
TEHRAN (IQNA)- Januari 19 inatambuliwa katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni "Siku ya Ghaza" kwa mnasaba wa kumbukumbu ya vita vya siku 22 vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza (Gaza) huko Palestina.

Utawala ghasibu wa Kizayuni unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu Disemba 27 mwaka 2008 ulianzisha vita dhidi ya Ghaza; ambavyo vilimalizika tarehe 17Januari 2009 baada ya kudumu kwa siku 22. Kwa mujibu wa makadirio ya Kituo cha Haki za Binadamu na Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya raia wa Palestina waliouliwa shahidi katika vita hivyo ni kati ya  1,314 hadi 1,434. Kati ya mashahidi hao, watoto walikuwa 412 na wanawake 115. Aidha licha ya kusababisha maafa hayo ya kiroho, vita hivyo vya utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza viliharibu na kubomoa miundomsingi ya viwanda, uchumi na sekta ya afya sambamba na kulisababishia eneo hilo maafa na hasara nyingi ikiwa ni pamoja na kubomolewa nyumba za raia zaidi ya elfu ishirini. 

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Kwa msingi huo, kwa kuzingatia maafa  ya kiroho na uharibifu uliotekelezwa  katika vita vya Ghaza, yote hayo yanahesabiwa kuwa jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita zilizotekelezwa na utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Ukubwa wa hujuma na uhalifu uliofanywa na Israel dhidi ya wakazi wa Ghaza ulilipelekea Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwasilisha azimio na kuutuhumu utawala wa Kizayuni kwa kukiuka pakubwa haki za binadamu. Azimio hilo lilitaka kuhitimishwa mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina katika eneo hilo lililo chini ya mzingiro wa kiuchumi.  

Uchunguzi wa UN

Nukta nyingine ni hii kuwa, Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwaka 2009 iliunda kamati ya uchunguzi kuhusu vita hivyo vya sku 22 vya mwaka 2008 dhidi ya Ghaza na baada ya kufanya uchunguzi wake kwa muda wa miezi 5, Septemba 2009  iliwasilisha ripoti ya kurasa 574 kwa Baraza la Haki za Binadamu la UN. Ripoti hiyo ilieleza kuwa, Israel ilifanya uhalifu ambao ni sawa na jinai za kivita. Ripoti hiyo vile vile iliongeza kuwa, Israel ilitekeleza oparesheni za kijeshi dhidi ya wakazi wote wa Ukanda wa Ghaza ili kusogeza mbele sera zake endelevu na kuu lengo likiwa ni kuwaadhibu raia wa Kipalestina wa eneo hilo. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia tarehe 5 mwezi Novemba lilipasisha ripoti ya kamati ya uchunguzi kwa jina "Ripoti ya Richard Goldstone".  Pamoja na hayo, licha ya kutolewa ripoti hiyo ya wazi, lakini Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikuchukua hatua zozote dhidi ya utawala ghasibu wa Israel wala za kuisadia na kuiunga mkono Ghaza.  

Kimya cha Umoja wa Mataifa

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa ulinyamazia kimya ripoti ya Goldstone na jinai za utawala wa Kizayuni wakati wa kujiri vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza sambamba na kuzingirwa ukanda huo. Israel ilianza kuuzingira Ukanda wa Ghaza tokea mwaka 2006;  yaani ilikuwa imepita miaka miwili tangu kuzingirwa eneo hilo pale kulipojiri vita vya siku 22 vya Israel dhidi ya wakazi wa eneo hilo; ambapo vyombo vya habari na weledi wengi wa mambo wameitaja Ghaza kuwa gereza kubwa zaidi la wazi kuwahi kushuhudiwa duniani. 

Hitilafu za Wapalestina

Hapa kuna nukta nyingine muhimu ambayo inaweza kuwa ibra na funzo kwa Wapalestina; nayo ni kuwa, Ukanda wa Ghaza ulitwishwa vita vya mwaka 2008 kufuatia kupamba moto hitilafu kati ya makundi ya Palestina. Mzozo na mvutano ulijitokeza kati ya Harakati za Fat-h na Hamas baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kushinda uchaguzi wa bunge mwaka 2006 na kuunda serikali chini ya uongozi wa Ismail Hania; ambapo utawala haramu wa Kizayuni pia ulistafidi na mzozo huo na kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Ghaza lengo likiwa eti kuiunga mkono harakati ya Fat-h na kushadidisha hitilafu kati ya Wapalestina. 

Iran inaunga mkono ukombozi wa Palestina

Sasa imepita miaka 15 tokea kujiri vita mwaka 2008 na miaka 17 hadi sasa tokea Wazayuni wauzingire Ukanda wa Ghaza. Ukanda huo unaendelea kuwa gereza kubwa zaidi la wazi kuwahi kushuhudiwa duniani huku wakazi wake wakiendelea kutaabika na matatizo mbalimbali ikiwa ni natija ya  mzingiro huo wa kiuchumi. Katika hali ambayo nchi za Kiarabu zimekaa kimya na kutochukua hatua mkabala wa jinai za utawala ghasibu wa Israel; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuiunga mkono pakubwa  Palestina na Ghaza; kama ambavyo imeamua kuipa katika kalenda yake jina la "Siku ya Ghaza" kila ifikapo tarehe 19 Januari. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 2008 iliunga mkono pia ushujaa uliodhihirishwa na wananchi wa Palestina katika vita hivyo. Kuhusiana na hilo, Hani al Thawabtah mwakilishi wa ngazi ya juu wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina amemueleza ripota wa Iran Press huko Ghaza kwamba: Hatua ya Iran ya kutenga siku maalumu kwa jina la  "Siku ya Ghaza" inadhihirisha kuendelea uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa malengo ya Palestina.  

Iranpress

 

captcha